MOSHI-KILIMANJARO
Mratibu wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu Kanda ya Kaskazini, Frederick Sumaye, amewataka wakazi wa mkoa wa Kilimanjaro, kujitokeza kwa wingi kupiga kura siku ya Oktoba 29, 2025, huku akiwahakikishia kuwa hali ya usalama imeimarishwa kikamilifu katika kipindi chote cha uchaguzi.
Akizungumza Oktoba 27, 2025, mjini Moshi, wakati akifunga mkutano wa kampeni za Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa Jimbo la Moshi Mjini, uliofanyika katika Stendi Ndogo ya Vumbi, mkoani Kilimanjaro, Sumaye aliwahimiza wananchi wa jimbo hilo kujitokeza kwa wingi kwenda kupiga kura.
Amesema Jimbo la Moshi Mjini lina jumla ya wapiga kura 167,000 waliandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, na amewaomba wananchi wote kutoa kura za ushindi kwa mgombea urais wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan.
“Nawaomba watu wote wa Jimbo la Moshi Mjini mliojiandikisha wapiga kura 167,000, angalau kura 165,000 ziende kwa Chama cha Mapinduzi, tuwape ushindi wa kishindo,” alisema Sumaye.
Aidha, Sumaye alisema Kanda ya Kaskazini inajumuisha majimbo 23, na akalisisitiza Jimbo la Moshi Mjini kuongoza kwa kura nyingi za urais, akieleza kuwa Rais Samia amefanikisha maendeleo makubwa katika sekta za afya, elimu, maji, barabara, nishati, kilimo, utalii na uwekezaji.
Sumaye, ambaye pia ni Waziri Mkuu mstaafu, aliongeza kuwa Rais Samia alifurahishwa na mapokezi makubwa ya heshima aliyopewa na wakazi wa Moshi Mjini wakati wa ziara yake, na akawataka wakaazi hao kuonyesha heshima hiyo kwa kujitokeza kwa wingi siku ya Oktoba 29, mwaka huu, kumpigia kura yeye pamoja na wagombea wa CCM wa ubunge na udiwani.


















