SHAYO AWAHIDI WAKAZI WA MOSHI MJINI KUSIMAMIA UKAMILISHAJI WA UWANJA WA NDEGE, STENDI MPYA YA NGANGAMFUMUNI

MOSHI-KILIMANJARO

Mgombea ubunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika Jimbo la Moshi Mjini, Ibrahim Shayo, amewataka wananchi wa jimbo hilo kumpa kura katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025, ili aweze kushirikiana na Serikali katika kutatua changamoto zinazolikabili jimbo hilo, ikiwemo ukamilishaji wa uwanja wa ndege wa Moshi na stendi mpya ya mabasi ya Ngangamfumuni.

Akizungumza Oktoba 27, 2025, wakati wa mkutano wa kufunga kampeni za CCM uliofanyika katika stendi ya vumbi Moshi mjini, Shayo alisema kukamilika kwa uwanja wa ndege wa Moshi kutachochea ukuaji wa sekta ya utalii, kwani mji huo ni lango kuu la Mlima Kilimanjaro na kivutio kikubwa kwa watalii kutoka mataifa mbalimbali.

“Nikipewa ridhaa ya kuwa mbunge wenu, nitapigania Serikali ikamilishe uwanja wa ndege wa Moshi ili kukuza biashara ya utalii na kuongeza ajira kwa vijana,” alisema Shayo.

Aidha, Shayo aliahidi kushirikiana na Serikali kuhakikisha mradi wa stendi mpya ya mabasi ya Ngangamfumuni, ambao umekuwa ukisuasua kwa muda mrefu, unakamilika haraka ili kuwapa wafanyabiashara na abiria mazingira bora ya kufanya shughuli zao.

Pia alisema atahakikisha ujenzi wa hospitali ya wilaya inayojengwa katika Kata ya Ng’ambo unakamilika kwa wakati, ili wananchi wa Moshi mjini wapate huduma za afya kwa ukaribu na ubora unaostahili.

“Tunataka Moshi ibaki kuwa mji wa mfano nchini kwa maendeleo, tukiunganisha nguvu, tutakamilisha miradi yote hii,” aliongeza Shayo.











Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.