MOSHI-KILIMANJARO.
Mgombea Udiwani wa Kata ya Mawenzi, Apaikunda Naburi, amewaomba wananchi wa kata hiyo kumpa tena ridhaa ya kuongoza kwa awamu nyingine, akisisitiza kuwa katika kipindi chake cha uongozi amefanikisha miradi mingi ya maendeleo.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika viwanja vya Posta mjini Moshi, mkutano ulihudhuriwa pia na Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Moshi Mjini, Theresia Komba, Naburi alisema ameongoza juhudi mbalimbali zilizoleta mafanikio makubwa katika kata hiyo.
Alitaja baadhi ya mafanikio hayo kuwa ni ujenzi wa Ofisi ya Mtendaji Kata, ambayo awali haikuwepo, ujenzi wa madarasa katika Shule ya Msingi Uhuru, na ukarabati wa Shule ya Msingi Mwenge.
Aidha, alieleza kuwa katika kipindi chake pia alisimamia ukarabati wa Kituo cha Walimu Moshi, ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mawenzi, pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama katika kata hiyo.
Katika upande wa utunzaji wa mazingira, Naburi alisema ameweka mikakati madhubuti iliyowezesha Mtaa wa Rengua, uliopo ndani ya Kata ya Mawenzi, kushika nafasi ya kwanza kitaifa kati ya mitaa yote nchini Tanzania.
Akizungumzia vipaumbele vyake endapo atachaguliwa tena, Naburi alisema ataweka mkazo katika kuhakikisha kata hiyo inakuwa na taa za barabarani.
“Kata ya Mawenzi inapokea watalii wengi wanaokuja kupanda Mlima Kilimanjaro, lakini inapofika usiku mji unakuwa gizani, nipeni kura nihakikishe taa za barabarani zinawekwa,” alisema Naburi.
Aidha, aliahidi kushughulikia kero ya mifereji ya maji ya mvua, akisema ni moja ya changamoto zinazowakabili wakazi wa kata hiyo.
Apaikunda Naburi ni mgombea pekee mwanamke aliyethubutu kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo kwa mara ya pili, na kuibuka mshindi dhidi ya wanaume katika mchakato wa kura za maoni ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), hivyo kuteuliwa tena kugombea Udiwani wa Kata ya Mawenzi.








