MOSHI-KILIMANJARO
Wagombea wa nafasi ya udiwani katika Halmashauri ya Manispaa ya Moshi wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuleta fedha nyingi za miradi ya maendeleo katika jimbo hilo.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni wa mgombea udiwani wa Kata ya Mawenzi, Apaikunda Naburi, uliofanyika Oktoba 25, 2025 katika viwanja vya Posta mjini Moshi, mgombea udiwani wa Kata ya Korongoni kwa tiketi ya CCM, Issa Elias Bulilo, alisema Serikali ya Awamu ya Sita imeboresha maisha ya wananchi kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Bulilo alisema kuwa katika kipindi kifupi, Serikali imetoa Sh bilioni 2 kwa ajili ya ujenzi wa jengo jipya la huduma za upasuaji katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mawenzi (MRRH) iliyopo Kata ya Mawenzi.
Alieleza kuwa mgombea udiwani wa kata hiyo, Apaikunda Naburi, ambaye pia ni Katibu wa Kamati ya Maendeleo ya Kata, amesimamia vyema utekelezaji wa fedha hizo ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati.
“Ujenzi huu ni sehemu ya mwendelezo wa maboresho ya sekta ya afya yanayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia, yenye lengo la kusogeza huduma bora za afya karibu zaidi na wananchi,” alisema Bulilo.
Aliongeza kuwa jengo hilo litakuwa na huduma za kisasa, ikiwemo huduma ya kusafisha figo (dialysis) kwa wagonjwa wanaohitaji matibabu hayo, hatua itakayopunguza changamoto za huduma za afya kwa wananchi wa Moshi na maeneo jirani.
Kwa upande wake, mgombea udiwani wa Kata ya Miembeni, Haruna Ally Mushi, aliishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa fedha za miradi ya maendeleo, hasa katika sekta ya afya, elimu na miundombinu.
Mushi aliwaomba wananchi wa Kata ya Mawenzi kumpigia kura mgombea udiwani wao, Apaikunda Naburi, ili aendelee kusimamia miradi ya maendeleo katika kata hiyo.
Aidha, aliwaomba wananchi wote jimboni Moshi Mjini kuwachagua wagombea wa CCM akiwemo Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Mgombea Ubunge wa Jimbo la Moshi Mjini, Ibrahim Shayo, pamoja na madiwani wote wa chama hicho, ili kuendeleza kasi ya maendeleo katika jimbo hilo.












