VIKUNDI VYA FLORESTA VYAWEKA AKIBA YA SH BILIONI 4

MOSHI-KILIMANJARO.

Vikundi 95 vya kuweka na kukopa vinavyosimamiwa na Shirika lisilo la kiserikali la Floresta Tanzania vimefanikiwa kuweka akiba ya shilingi bilioni 4 na kutoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 2.6, hatua iliyowezesha wanachama wake kuboresha ustawi wa kiuchumi katika ngazi ya kaya.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Afisa Uhusiano wa Floresta Tanzania, Brenda Kuringe, shirika hilo linatarajia kuhitimisha rasmi shughuli zake Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro baada ya miaka 20 ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kijamii na mazingira.

“Kupitia vikundi hivi, wanachama wapatao 2,500 wamepata nafasi ya kujiwekea akiba, kupata mikopo na kuanzisha miradi ya kiuchumi iliyosaidia kuongeza kipato na kupunguza utegemezi katika familia,” alisema Kuringe.

Alisema sherehe za kufunga rasmi shughuli hizo zitafanyika katika Hotel ya African Flower, iliyopo Mji Mdogo wa Himo wilayani humo, zikihudhuriwa na mkuu wa wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, ambapo kutakuwa na maonesho ya vikundi vya wanachama na ushuhuda kutoka kwa wananchi waliokuwa wanufaika wa miradi hiyo.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa kwa kipindi cha miaka 20 ya utekelezaji, Floresta Tanzania imefanikiwa kuanzisha ushirikiano na taasisi zaidi ya 100 za elimu ikiwemo shule za msingi, sekondari na vyuo, kwa lengo la kuwafikia watoto na vijana kupitia elimu ya uhifadhi wa mazingira na ujasiriamali.

Pia alisema wameweza kushirikiana na taasisi 77 za dini (makanisa na misikiti) kufanikisha urejesho wa mahusiano kati ya Mungu, mwanadamu na mazingira, hatua iliyosaidia kufikia wanajamii wengi zaidi nje ya vikundi vya kijamii.

Alisema.katika kipindi hicho asilimia 85 ya wanachama wake walifanikiwa kuanzisha miradi mbalimbali ya kiuchumi, jambo lililoongeza vyanzo vya mapato na kudhibiti matumizi katika kaya.

Vile vile alisema katika kipindi cha miaka 20 waliweza kupanda zaidi ya miche 200,000 ya miti kila mwaka katika maeneo mbalimbali ikiwemo vyanzo vya maji, mito, mabonde na mashamba binafsi, ili kuhifadhi udongo, kurejesha rutuba na kuimarisha uoto wa asili

Piq walitoa elimu ya kilimo hai, ambapo zaidi ya asilimia 80 ya wakulima walionufaika wameongeza mavuno, chakula na kipato kwa familia zao.

Alisema kwa kipindi hicho cha miaka 20, shirika hilo limeendelea kutekeleza shughuli zake kupitia programu tatu kuu ikiwemo makuzi ya kiuchumi, utunzaji na uhifadhi wa mazingira, pamoja na makuzi ya kiroho, ambazo zimekuwa zinatekelezwa katika kata 10 za Wilaya ya Moshi.

"Kupitia programu hizi, Floresta imechangia kwa kiasi kikubwa katika kuboresha maisha ya wananchi, kukuza uelewa wa uhifadhi wa mazingira, na kuimarisha uchumi wa kaya,” aliongeza Kuringe.

Floresta Tanzania ilianzishwa mwaka 2004 kwa lengo la kuhifadhi mazingira na kupunguza umaskini nchini Tanzania, hususan katika jamii za vijijini ikiwemo Wilaya ya Moshi.








Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.