MOSHI-KILIMANJARO.
Uzinduzi wa Mwanga Utalii Festival msimu wa tatu unatarajiwa kufanyika kesho, Novemba 14, katika kata ya Lang’ata, wilayani Mwanga, mkoani Kilimanjaro.
Uzinduzi huo utafanyika katika ufukwe wa Bwawa la Nyumba ya Mungu, Lang’ata, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Afisa Utalii wa Wilaya ya Mwanga, Hellena Majagi, huku wadau mbalimbali wa utalii akiwemo wawakilishi kutoka TFS (Tanzania Forest Services Agency) wakihudhuria.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Mwanga Utalii Festival, Frida Mberesero, alisema lengo la mbio hizo ni kutangaza vivutio vya utalii vilivyomo ndani ya Wilaya ya Mwanga ambavyo havijatangazwa vya kutosha.
"Wilaya ya Mwanga imebarikiwa kuwa na vivutio vingi vya kipekee kama vile mapango yenye mafuvu ya watu wa kale yaliyopo Kisangara Juu, vivutio vya ufukweni, maporomoko ya maji, na maeneo ya kihistoria kama mawe ya Mkumbavana,” alisema Mberesero
Alifafanua kuwa mapango ya Kisangara Juu yanahusiana na historia ya kale ambapo wakati huo, mtu alipofariki dunia, alikatwa kichwa na kubakizwa mwili pekee kuzikwa, huku kichwa kikihifadhiwa mapangoni jambo ambalo kwa sasa limebaki kuwa historia.
Aidha, alitaja vivutio vingine vya kihistoria kama mawe ya Mkumbavana, ambapo zamani iliaminika mtoto aliyezaliwa na ulemavu wa viungo alipelekwa eneo hilo na kutupwa ili kuondoa mkosi katika familia historia ambayo sasa inavutia watafiti na watalii wa ndani na nje ya nchi.
“Kupitia Mwanga Utalii Festival-2025, tunalenga kuibua maeneo haya yasiyotangazwa vya kutosha, ili serikali iweze kuyaboresha na kuwanufaisha wananchi kiuchumi kupitia utalii wa ndani,” aliongeza.
Kwa mujibu wa Mberesero, kilele cha Mwanga Utalii Festival msimu wa tatu kitafanyika Desemba 27 mwaka huu katika uwanja wa C.D-Msuya, ambapo kutakuwa na mbio za kilomita 10, kilomita 5, na kilomita 2.5 kwa watoto na wazee, pamoja na mbio za baiskeli za kilomita 60.
Pia, katika siku hiyo kutakuwa na maonesho mbalimbali ikiwemo utalii wa vyakula na vinywaji vya asili, nyama choma, ngoma za asili, na bidhaa za wajasiriamali kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa wa Kilimanjaro.
Mberesero alihitimisha kwa kusema kuwa festival hiyo inalenga kuunganisha jamii katika kutangaza utalii, kukuza uchumi wa wananchi, na kulinda urithi wa utamaduni wa Mwanga.






