TAMASHA LA UTALII LAZINDULIWA, WADAU WAIOMBA SERIKALI KUJENGA BARABARA

MWANGA-KILIMANJARO. 

WADAU wa utalii wilayani Mwanga, mkoani Kilimanjaro, wameiomba Serikali kuboresha barabara zinazoelekea kwenye maeneo yenye vivutio vya utalii ili kurahisisha safari za wageni wanaotembelea maeneo hayo.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Kampuni ya Utalii ya Kisangara Bi. Frida Mberesero, wakati wa uzinduzi wa Tamasha la Mwanga Utalii Festival, lilofanyika Novemba 14, 2025 Ufukweni mwa Bwawa la Nyumba ya Mungu lililopo Kata ya Lang’ata Wilayani humo.

Frida amesema ubovu wa barabara umekuwa kikwazo kikubwa kwa wadau wa utalii kuwafikisha watalii kwenye vivutio mbalimbali, jambo linalosababisha kutopatikana kwa fursa nyingi za kiuchumi na kijamii.

“Changamoto ya barabara imekuwa ikiturudisha nyuma, tunaiomba Serikali kuboresha miundombinu hii kwa sababu ni hatua muhimu katika kukuza utalii na uchumi wa vijiji vinavyounganishwa na barabara hizi,” amesema.

Akizungumzia utalii wa ufukweni, amesema una faida nyingi na una uwezo wa kuvutia wageni wengi wa ndani na nje ya nchi kutembelea maeneo yenye fukwe.

Ameongeza kuwa Bwawa la Nyumba ya Mungu ni miongoni mwa vivutio muhimu vya utalii wa ndani, huku akiwahamasisha wananchi kulitembelea.

“Bwawa hili lina vivutio vingi, ikiwemo shughuli za uvuvi, shughuli za umwagiliaji na uzalishaji wa umeme, hivyo ni rasilimali muhimu ambayo ikitangazwa vizuri itazalisha kipato kwa jamii,” amesema.

Akizindua Tamasha hilo, Afisa Utalii wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, Bi. Hellena Majagi, amempongeza  Frida Mberesero kwa juhudi zake za kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo wilayani humo, hatua inayochochea mwamko wa utalii wa ndani.

“Tunamshukuru sana Mkurugenzi wa Kisangara Tours kwa kuendelea kuhamasisha utalii wa ndani, tuna vivutio vingi ambavyo bado havijatangazwa vya kutosha; uwepo wa tamasha hili ni fursa muhimu ya kuvitangaza vivutio vyetu,” amesema Majagi.

Aidha, ameishukuru Serikali kwa kufungua Lango la Utalii la Ndea, akisema hatua hiyo itachochea zaidi ukuaji wa utalii ndani ya Wilaya ya Mwanga.

Bi. Majagi amebainisha kuwa wilaya hiyo ina vivutio mbalimbali vya utalii, ikiwemo maeneo ya kihistoria, Ziwa Jipe na Bwawa la Nyumba ya Mungu.

Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Lang’ata Bora, ambako tamasha hilo limezinduliwa, wamepongeza juhudi hizo huku wakisema kuwa zitafungua fursa zaidi za utalii wa ufukwe katika Bwawa la Nyumba ya Mungu ambalo bado halijatangazwa vya kutosha.











Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.