UJENZI WA BWAWA LA KUNYWESHEA MIFUGO LANGAI WAFIKIA ASILIMIA 92

SIMANJIRO.

UJUNZI wa bwawa la kunyweshea mifugo katika Kijiji cha Langai wilayani Simanjiro, mkoani Manyara, umefikia asilimia 92, huku serikali ya wilaya hiyo ikimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa shilingi milioni 700 kutekeleza mradi huo muhimu kwa wafugaji.

Akizungumza jana wakati wa kukagua maendeleo ya ujenzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Faki Lulandala, amesema ameridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi na kupongeza juhudi za serikali katika kuleta miradi inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.

Amesema bwawa hilo litakuwa na uwezo wa kuhifadhi maji muda wote wa mwaka na kuondoa adha ya wananchi na mifugo kutembea umbali mrefu wakitafuta huduma hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Pangani, Mhandisi Segule Segule, amesema bwawa hilo sasa lina uwezo wa kuhudumia zaidi ya mifugo 380,000 kwa mwaka, ikilinganishwa na uwezo wa awali wa mifugo 10,000 pekee.

Aidha, sambamba na bwawa hilo, mbaruti ya kuchotea maji kwa wananchi pia imejengwa ili kuepusha wananchi kuingia kwenye bwawa.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Langai, Michael Philipo, ameishukuru serikali kwa kuendelea kuleta miradi muhimu kijijini hapo, ikiwemo mradi wa maji safi wenye thamani ya shilingi milioni 800, josho la mifugo, ghala la mazao na umeme wa REA.

Ujenzi wa bwawa hilo unatekelezwa na mkandarasi Eker Limited chini ya usimamizi wa wataalamu kutoka Wizara ya Maji na Bodi ya Maji Bonde la Pangani.








Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.