LANGO LA NDEA LACHOCHEA UKUAJI WA UTALIII MWANGA

LANG'ATA-MWANGA.

AFISA Utalii wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, Hellena Majagi, ameishukuru Serikali kwa kufungua lango la kuingilia na kutoka watalii la Ndea, lililopo Kijiji cha Karambandea, Tarafa ya Toroha ndani ya Hifadhi ya Taifa Mkomazi, akisema hatua hiyo itachochea ukuaji wa sekta ya utalii wilayani humo.

Majagi aliyasema hayo jana wakati wa uzinduzi wa Tamasha la Mwanga Utalii Festival, lililofanyika katika ufukwe wa Bwawa la Nyumba ya Mungu lililopo Kata ya Lang’ata.

Amesema ujenzi wa lango hilo umeongeza idadi ya watalii wanaotembelea mbuga hiyo, ambapo wengi huvutiwa na maisha ya jamii ya Ziwa Jipe, Faru Weusi, Tembo, Nyati Twiga, Ndege na Swala wanaopatikana ndani ya Hifadhi ya Taifa Mkomazi.

"Lango hili limechochea fursa za kiuchumi kwa wananchi wanaozunguka eneo la hifadhi kutokana na ongezeko la watalii wanaopita njia hiyo, pamoja na kutengeneza ajira kwa wakazi wa vijiji jirani,” alisema Majagi.

Alieleza kuwa ujenzi wa lango hilo ni sehemu ya maboresho makubwa yaliyofanywa na Serikali ya awamu ya sita katika kuboresha na kuongeza vivutio vya utalii nchini.

Afisa huyo pia alimpongeza Mkurugenzi wa Kampuni ya Utalii ya Kisangara Tours, Frida Mberesero, kwa juhudi zake za kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo wilayani humo, hatua inayoongeza mwamko wa utalii wa ndani.

“Tunamshukuru sana Mkurugenzi wa Kisangara Tours kwa kuendelea kuhamasisha utalii wa ndani. Tuna vivutio vingi ambavyo bado havitangazwi vya kutosha; uwepo wa tamasha hili ni fursa muhimu ya kuvitangaza,” alisema Majagi.

Alibainisha kuwa Wilaya ya Mwanga inayo vivutio vingi vya utalii, ikiwemo maeneo ya kihistoria, Ziwa Jipe, Bwawa la Nyumba ya Mungu, Hifadhi ya Taifa Mkomazi, maporomoko ya maji na maeneo ya misitu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kisangara Tours, Frida Mberesero, ameomba Serikali kuboresha barabara zinazoelekea kwenye vivutio vya utalii ili kurahisisha safari za wageni wanaotembelea maeneo hayo.

Alisema ubovu wa miundombinu hiyo umekuwa kikwazo kikubwa kwa wadau wa utalii kuwafikisha watalii kwenye maeneo husika, jambo linalosababisha kukosekana kwa fursa nyingi za kiuchumi na kijamii.

“Changamoto ya barabara imeturudisha nyuma. Tunaiomba Serikali kuboresha miundombinu hii kwa sababu ni hatua muhimu katika kukuza utalii na uchumi wa vijiji vinavyounganishwa na barabara hizi,” alisema.

Akizungumzia utalii wa ufukweni, Mberesero alisema kuwa una faida nyingi na una uwezo wa kuvutia wageni wa ndani na nje ya nchi.

Aidha, aliongeza kuwa Bwawa la Nyumba ya Mungu ni miongoni mwa vivutio muhimu vya utalii wa ndani na akawataka wananchi kujenga utamaduni wa kulitembelea.

Nso baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Lang’ata Bora, ambako tamasha hilo limezinduliwa, wamepongeza juhudi hizo, wakisema zitafungua fursa zaidi za utalii wa ufukweni katika Bwawa la Nyumba ya Mungu ambalo bado halitangazwi vya kutosha.

Tamasha la Mwanga utalii litafanyika Desema 27, mwaka huu katika uwanja wa C.D Msuya, ambapo kutakuwa na maonesho mbalimbali vikiwemo vyakula vya asili, ngoma, maonesho ya wajasiriamali, matembezi ya kilomita 2.5 kwa watoto na wazee, matembezi ya kilomita 10 pamoja na kuendesha baiskeli umbali wa kilomita 60.






Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.