MOSHI-KILIMANJARO.
Mgombea udiwani wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Kiboriloni, Manispaa ya Moshi, Willy Tully, ameahidi kushughulikia changamoto ya muda mrefu ya mwingiliano wa mipaka kati ya Manispaa ya Moshi na Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Vijijini, hasa katika maeneo yanayohusiana na anuani za makazi.
Akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika Oktoba 12,2025 katika Mtaa wa Mnazi, Tully alisema mtafaruku huo umesababisha mkanganyiko kwa wakazi wa maeneo ya mipakani kama vile Mtaa wa Kaanani (KKKT), ambapo nyumba zao zimewekewa namba za anuani za makazi na halmashauri zote mbili.
"Wananchi wa Kaanani hawafahamu kama wako Manispaa au Moshi Vijijini, hii siyo haki, nikipewa ridhaa, nitafuatilia suala hili kwa karibu kwenye mamlaka husika ili pawe na mipaka ya wazi na kuondoa usumbufu huu,” alisema Tully.
Mgombea huyo alieleza kuwa mipaka isiyoeleweka inasababisha ukosefu wa huduma bora kwa wananchi na inaweza hata kuathiri upangaji wa bajeti na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kata hiyo.
Akitaja changamoto nyingine zinazowakabili wananchi wa Kiboriloni, Tully alieleza kuwa mpaka kati ya Mtaa wa Mnazi na Bekari kupitia barabara maarufu ya Mnazi–Bekari bado ni eneo la mgogoro, kwani kila upande unadai ni mali ya halmashauri yake.
“Tutakapoingia kwenye Baraza la Madiwani, tutaweka nguvu kuhakikisha migogoro hii ya mipaka inapatiwa ufumbuzi wa kudumu. Wananchi hawastahili kubaki kwenye sintofahamu ya kiutawala,” aliongeza.
Aidha, Tully ameahidi kushughulikia matatizo ya usalama kwenye maeneo ya soko la Kiboriloni Center, ambapo ameeleza kuwepo kwa vibaka wanaowahangaisha wananchi, hasa wakati wa jioni.
Ameeleza pia kuwa soko la mazao lililopo eneo la KDC linakabiliwa na uhaba mkubwa wa miundombinu muhimu ikiwemo ya maji na vyoo, jambo linalosababisha wafanyabiashara kujisaidia kwenye mashamba ya watu, hali inayohatarisha afya ya jamii.
“Soko hili halina hata huduma ya maji wala choo, nikichaguliwa, nitahakikisha linawekwa miundombinu ya msingi ili wafanyabiashara wafanye shughuli zao kwa heshima na usafi,” alisema.
Tully pia aligusia uharibifu wa miundombinu ya maji uliosababishwa na mafuriko ya hivi karibuni na kuahidi kuwa, atapigania mamlaka husika kuhakikisha huduma hiyo inarudi haraka.
Changamoto nyingine aliyoitaja ni hali ya barabara za ndani ambazo zinahitaji ukarabati mkubwa ili kurahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa ndani ya kata hiyo.
Mgombea huyo amewaomba wananchi wa Kiboriloni kumpa kura Oktoba 29, mwaka huu, ili aweze kutimiza dhamira yake ya kuleta maendeleo ya kweli na kutatua changamoto zinazowakabili kwa muda mrefu.
“Ninawaomba mnichague kuwa Diwani wenu. Sitawaangusha, nitapigania haki zenu kwa nguvu zote,” alisisitiza.










