MGOMBEA UBUNGE IBRAHIM SHAYO: "NIKICHAGULIWA, STENDI YA NGANGAMFUMUNI ITAKAMILIKA NDANI YA MIAKA MITANO"

MOSHI-KILIMANJARO.

Mgombea ubunge wa Jimbo la Moshi Mjini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Ibrahim Mohamed Shayo, ameahidi kuhakikisha kuwa ujenzi wa stendi ya mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani ya Ngangamfuni, unakamilika ndani ya kipindi chake cha miaka mitano, iwapo atachaguliwa katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, mwaka huu.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Oktoba 12, 2025 katika mtaa wa Sokoni, Kata ya Mjimpya, Shayo aliwaomba wananchi kumpa kura ili aweze kwenda kupigania kukamilika kwa stendi hiyo muhimu, ambayo imekuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu na wakazi wa Moshi.

"Naombeni kura zenu Oktoba 29 mwaka huu, niende nikapambane ile stendi ya Ngangamfuni iweze kukamilika. Nawaahidi ndani ya kipindi changu cha miaka mitano stendi hii itakamilika na kuanza kutoa huduma. Kama haitakamilika, nikiomba tena kura msinichague," alisema Shayo kwa msisitizo.

"Stendi hiyo ya kisasa inajengwa katika Kata ya Ngangamfuni, Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, hata hivyo, mradi huo umesimama tangu Mei 2022 kutokana na ukosefu wa fedha, hali iliyosababisha ucheleweshwaji mkubwa wa maendeleo ya ujenzi huo."

Kwa mujibu wa Shayo, alisema ujenzi wa stendi ulianza Januari 28, 2019 na ulitengewa kiasi cha Shilingi bilioni 28.8, hata hivyo, kutokana na kusimama kwa miezi 22, gharama za mradi zimeongezeka kwa Shilingi milioni 565.

Akitolea mfano, Shayo alisema stendi zingine kama ile ya Magufuli na Nyamhongolo (Mwanza), ambazo zilianza kujengwa kwa wakati mmoja, tayari zimekamilika na zinafanya kazi, huku stendi ya Moshi ikiwa bado haijakamilika.

Alieleza kuwa kukamilika kwa stendi hiyo kutakuwa na faida kubwa kwa wakazi wa Moshi, ikiwemo kuongeza ajira kupitia biashara zitakazofanyika ndani ya kituo hicho pamoja na nafasi mbalimbali za ajira zitakazotolewa.

"Stendi hii ikikamilika, itahudumia mabasi 300 kwa siku na kati ya hayo, 72 yataweza kuegeshwa kwa wakati mmoja. Pia kutakuwa na ofisi, migahawa, hoteli, maegesho ya magari binafsi 218, teksi 34, pamoja na maeneo ya bajaji na bodaboda 20," alifafanua Shayo.

Alisema kama atapewa ridhaa na wananchi pamoja na madiwani wa CCM, atahakikisha hoja ya kukamilisha stendi hiyo inapelekwa kwenye Baraza la Madiwani na kufanyiwa kazi haraka iwezekanavyo.




Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.