MOSHI-KILIMANJARO.
Mgombea ubunge wa Jimbo la Moshi Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ibrahim Shayo, ameahidi kushughulikia changamoto ya uchakavu wa mfumo wa majitaka, miundombinu mibovu ya barabara na taa za mtaa katika Kata ya Kilimanjaro, endapo atachaguliwa kuwa mwakilishi wa wananchi bungeni.
Akizungumza Oktoba 11, 2025 katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika Kata ya Kilimanjaro, Shayo alisema changamoto ya majitaka ni kubwa, ikiwemo kutokuwepo kwa mfumo rasmi wa maji taka kwenye kata nyingi ndani ya jimbo hilo, huku baadhi ya maeneo yakitumia vyoo vya mashimo ambayo ni vya zamani na yasiyo salama kwa mazingira.
“Hata mimi nyumbani kwangu bado natumia choo cha mashimo ya zamani, hili ni tatizo kubwa, kata nyingi za Manispaaya ya Moshi, hazina kabisa mfumo wa maji taka,” alisema Shayo.
Aliahidi kushirikiana na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA) kuhakikisha mabomba chakavu yanaondolewa na miundombinu mipya ya majitaka inawekwa ili kupunguza uchafuzi wa mazingira na kulinda afya za wakazi.
“Ni aibu kwamba Kata ya Kilimanjaro, ambayo ina hoteli nyingi za hadhi na inapokea wageni wa kitaifa na kimataifa, haina mfumo wa maji taka unaofanya kazi. Maji machafu yanatiririka hovyo. Nichagueni niende bungeni, nitahakikisha hili linapatiwa ufumbuzi wa haraka,” alisisitiza Shayo.
Aliongezq kuwa "Miaka mingi mabomba ya majitaka yamelazwa bila matengenezo. Uchafu huo unavuja katika makazi ya watu, na kusababisha malalamiko mengi, huu ni uzembe ambao lazima ukomeshwe,” alisema.
Mbali na hilo, aliahidi kuweka taa za barabarani katika maeneo ya giza ya kata hiyo ili kuongeza usalama kwa wakazi, hususan kwenye barabara ya Lema Road hadi International School, Kisinane–Mapipa, na Shant Town hadi Longuo.
Shayo pia alizungumzia changamoto ya barabara za ndani kuwa katika hali mbaya, akiahidi kuwa atasukuma mamlaka husika kuzitengeneza ili ziweze kupitika majira yote ya mwaka.
Kwa upande mwingine, Shayo aligusia suala la usalama lililowasilishwa na mgombea udiwani wa Kata ya Kilimanjaro, Ghulamhusein, akisema kuwepo kwa vibaka wanaopora wananchi na watalii kunahitaji hatua za haraka.
“Naomba mnichague mimi Ibrahim Shayo, pamoja na diwani wa CCM Kata ya Kilimanjaro, tutashirikiana kuhakikisha kituo cha polisi kilicholala kwa miaka mingi tunakifufua na ulinzi wa wananchi unaimarishwa,” aliongeza.
Uchaguzi mkuu unatarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025, ambapo Watanzania watapata nafasi ya kuwachagua viongozi watakaowaongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.















