MOSHI-KILIMANJARO
Mgombea wa nafasi ya udiwani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Kata ya Kilimanjaro, Ghulamhusein, ameahidi kushughulikia changamoto mbalimbali zinazoikabili kata hiyo ikiwemo kufufua kituo cha polisi kilichosimama kwa miaka mingi bila kufanya kazi ikiwa ni mikakati yake ya kuimarisha ulinzi na usalama wa kaziwa kata hiyo.
Akihutubia mkutano wa kampeni Oktoba 11, 2025, uliofanyika eneo la Shant Town, Moshi, mkoani Kilimanjaro, na kuhudhuriwa na mgombea ubunge wa Jimbo la Moshi Mjini, Ibrahim Shayo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Moshi Mjini Faraji Swai, Katibu wa Wilaya Amosi Shimba pamoja na Katibu Mwenezi Athuman Mfuchu.
Ghulamhusein alisema kituo cha polisi kilichopo katika kata hiyo kimeshindwa kufanya kazi kwa miaka mingi, hivyo amewaomba wananchi wa kata hiyo kumchagua ili aweze kwenda kushirikiana na mbunge kukifufua kituo hicho.
“Kituo chetu cha polisi hakifanyi kazi. Nitakapopewa ridhaa kuwa diwani, nitashirikiana na mbunge kuhakikisha tunakifungua kituo hicho ili wananchi wetu wawe na ulinzi wa uhakika dhidi ya vibaka wanaopora wakazi na hata watalii wanaolala kwenye hoteli zilizoko katika kata yetu,” alisema.
Aidha, Ghulamhusein alielezea kusikitishwa na ukosefu wa Ofisi ya CCM ya Kata hiyo tangu nchi ipate Uhuru, akisema kuwa katika kipindi chake cha miaka mitano, atahakikisha kata hiyo inapata ofisi ya kisasa itakayokuwa pia na mradi wa kiuchumi unaowezesha chama kupata mapato na vijana kupata ajira.
“Sio kila siku kwenda kwa diwani au mbunge kuomba fedha. Ofisi hiyo ya CCM itakuwa na mradi wa kujitegemea, na mimi nina mpango tayari, ingawa kwa sasa sitaweka wazi ni mradi gani,” alisema.
Mgombea huyo pia aliahidi kupigania upatikanaji wa mikopo isiyo na riba kutoka halmashauri kwa makundi maalum yakiwemo ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, ili kuwawezesha kuinuka kiuchumi.
“Nitahakikisha kila mwenye sifa anapata mkopo, wananchi wanataka kuinuka kibiashara, nitawapigania hadi kila mmoja anufaike na mikopo hiyo ya halmashauri,” aliongeza.
Akihitimisha hotuba yake, Ghulamhusein alisisitiza kuwa hajagombea nafasi hiyo kwa sababu ya kutafuta umaarufu au mali, bali kutokana na dhamira yake ya dhati kusaidia wananchi wa kata ya Kilimanjaro.
“Nina kila kitu ninachokihitaji, mimi ni mfanyabiashara, lakini nimeamua kugombea kwa sababu nataka kuwatumikia wqnanchi wq kta yangu ya Kilimanjaro, naombeni mnichague, mnipe miaka mitano tu, na nitahakikisha naleta maendeleo ya kweli katika kata yetu,” alisema.
Uchaguzi mkuu wa nafasi ya Rais Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, mwaka huu kote nchini.
















