CCM YAWAOMBA WANANCHI KUWACHAGUA WAGOMBEA WAKE KWA AJILI YA MAENDELEO ENDELEVU


MOSHI-KILIMANJARO.

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimesema kinao wagombea waadilifu, wakiongozwa na mgombea urais Dk. Samia Suluhu Hassan, ambaye ametajwa kuwa mzalendo namba moja wa taifa kutokana na uchapakazi wake na utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo nchini.

Kauli hiyo ilitolewa Oktoba 6, 2025 na Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Best Simba, wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika katika Mtaa wa Relini, Kata ya Pasua, Manispaa ya Moshi.


Simba alisema katika kipindi cha miaka minne na nusu ya uongozi wa Dk. Samia, taifa limeshuhudia mafanikio makubwa katika sekta mbalimbali kupitia utekelezaji wa miradi ya kimkakati.

"Tumchague Dk. Samia Suluhu Hassan kwa maendeleo ya Tanzania, amefanikiwa kusimamia miradi mikubwa kama reli ya kisasa (SGR), Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere, na ujenzi wa viwanja vya ndege, ikiwemo ule wa Moshi ambao utasaidia kuinua uchumi wa mkoa huu," alisema Simba.

Aidha, Simba ambaye pia ni Mratibu wa Kampeni wa Wilaya ya Moshi Mjini, aliwaomba wananchi kuwachagua wagombea wote wa CCM kwa nafasi ya ubunge na udiwani, ili waweze kushirikiana na Rais katika kuharakisha maendeleo kwa wananchi.

"Namuombea kura mgombea ubunge wa Moshi Mjini, Ibrahim Shayo, ili aweze kusukuma miradi ya barabara za ndani ambazo bado ni changamoto, kukamilika kwa hospitali ya wilaya, ujenzi wa stendi ya kisasa ya Ngangamfumuni na uwanja wa ndege wa Moshi," alieleza.

Aliongeza kuwa kupitia viongozi wa CCM, wananchi wataweza kupata huduma bora za afya, miundombinu ya kisasa, ajira kwa vijana na fursa zaidi kwa wajasiriamali.

Simba alihitimisha kwa kuwasihi wananchi kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, 2025 siku ya uchaguzi mkuu, kuwapigia kura wagombea wa CCM ili kuhakikisha ndoto ya maendeleo endelevu inatimia kwa vitendo.









Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.