MGOMBEA UBUNGE MOSHI MJINI, AMUOMBEA KURA DK. SAMIA, AAHIDI KUSUKUMA MIRADI YA MAENDELEO

PASUA-MOSHI.

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Moshi Mjini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Ibrahim Shayo, amewaomba wananchi wa Moshi kumchagua Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ili aweze kukamilisha miradi mikubwa ya maendeleo inayoendelea katika Manispaa hiyo.

Akihutubia katika mkutano wa kampeni uliofanyika jana katika Mtaa wa Relini, Kata ya Bomambuzi, Shayo alisema serikali ya CCM haina nia ya kuona miradi ya maendeleo ikikwama au kuchelewa kukamilika, hivyo wananchi wanapaswa kuipa ridhaa iendelee kuiongoza nchi.

"Stendi mpya ya mabasi ya Ngangamfumuni ni ya kimataifa inapokamilika itahudumia zaidi ya mabasi 300 kwa siku, ambapo mabasi 72 yanaweza kuegeshwa kwa wakati mmoja, kutakuwa na ofisi, maduka, migahawa, hoteli na maegesho ya magari binafsi, hii ni fursa kubwa kwa wananchi wa Moshi," alisema Shayo.

Aidha, alitaja pia mradi wa uwanja wa ndege wa Moshi kuwa miongoni mwa miradi mikubwa yenye tija kiuchumi, akisema kukamilika kwake kutafungua mzunguko mkubwa wa fedha na kuongeza idadi ya watalii wanaokuja kupanda Mlima Kilimanjaro.

“Kukamilika kwa stendi na uwanja wa ndege kutachochea uchumi wa Moshi; madereva wa teksi, bodaboda, bajaji na akina mama wajasiriamali watanufaika kwa kiasi kikubwa, haya yote yanawezekana tukimchagua Dk. Samia Suluhu Hassan na wagombea wote wa CCM,” alisema Shayo.

Kwa upande wa changamoto za ndani ya Kata ya Bomambuzi, Shayo aliahidi kuzishughulikia, zikiwemo za miundombinu ya barabara na afya.

“Ninafahamu changamoto ya barabara ya M-Pesa; ni mbaya kiasi kwamba magari madogo hayawezi kufika majumbani, nitahakikisha Manispaa inanunua greda na tunajenga barabara hizi kwa kiwango cha lami, tukiweka pia taa za barabarani,” alieleza.

Kuhusu kituo cha afya cha Bomambuzi, Shayo alisema kinakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa uzio, chumba cha kuhifadhia maiti, na upungufu wa madaktari, aliahidi kushughulikia changamoto hizo endapo atapewa ridhaa ya kuwa mbunge.

“Nawaomba kwa moyo wa dhati, Oktoba 29, mjitokeze kwa wingi kupiga kura, namuombea kura za kishindo Dk. Samia Suluhu Hassan, nipigieni na mimi Ibrahim Shayo kuwa mbunge wenu, pamoja na Dogo Janja Juma Raibu Juma kwa nafasi ya udiwani,” alihitimisha.










Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.