MOSHI-KILIMANJARO.
Muu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu, amesema serikali mkoani humo, inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya kahawa, ili kuboresha uzalishaji wa zao hilo kutokana na umuhimu wake katika kukuza uchumi wa Taifa.
Babu aliyasema hayo jana (Jumatano), wakati wa uzinduzi wa msimu wa sita wa “Tamasha la Kahawa Festival-2025” uliofanyika Moshi, mkoani humo.
“Kahawa mbali na kukuza uchumi wa taifa pia ni muhimu katika kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja kupitia ajira na mapato yatokanayo zao hilo”, alisema
Alisema serikali tayari imefanya mambo mengi yanayolenga kukuza uzalishaji wa kahawa hapa nchini ikiwemo kuboresha huduma za ugani, pembejeo na miundo mbinu za umwagiliaji kwenye eneo la uzalishaji wa zao kahawa hapa nchini.
Akizungumzia tamasha hilo, Babu aliupongeza uongozi wa Bodi ya Kahawa nchini TCB pamoja na wadau wengine wa kahawa kwa kulianzisha jambo ambalo alisema linachangia kuunga mkono juhudi za serikali za kuboresha uzalishaji wa zao la kahawa.
“Nimeelezwa hapa ya kuwa maonyesho haya ya Kahawa Festival-2025 msimu wa sita yanalenga kuhamasiha vijana na wananchi wote kwa ujumla kutambua fursa ambazo zinaptaikana kupitia mnyororo mzima wa zao la kahawa, uamuzi huu ni mzuri maana utachangia kushirikisha watu wengi zaidi kwenye uzalishaji wa zao hili”, alisema.
Aidha alitoa rai kwa wale wote wanaojihusisha na uzalishaji wa kahawa, kuhakikisha wanaitunza miti ya zao hilo na pale inapolazimika kuiondoa wairudishie kwa haraka.
“Asitokee mtu akakata mti wa kahawa bila sababu za msingi na pale inapobidi basi aurudishie mara moja ili kasi ya kuongeza uzalishaji iendelee”, allisema.
Kwa upande Mkurugenzi mkuu wa Bodi ya Kahawa nchini (TCB) Primus Kimaryo, alisema Tamasha hilo limelenga kuhamasisha unywaji wa ndani wa kahawa , sambamba na kukuza soko la ndani la unywaji wa kahawa.
“Tamasha hili pia ni kiunganishi muhimu kati ya wadau wa kahawa ambao hutoka sehemu mbalimbali ambapo pamoja na mambo mengine hupata fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu unaohusiana na uzalishaji wa kahawa”, alisema Kimaryo.
Aidha alisema tamasha hilo pia linatoa fursa kwa washiriki kupata elimu mpya ya uzalishaji wa zao hilo ambapo alisema ni pamoja na teknoloia mpya za ukaangaji na utayarishaji wa kahawa.
“Pia washiriki watapata fursa ya kufanya mashindano mbalimbali yanayohusiana na zao la kahawa, jambo ambalo litachangia kuboresha uzalishaji wa kahawa katika ngazi mbalimbali kuanzia shambani, sokoni hadi kwa mnywaji”, alisema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tamasha la Kahawa Festival-2025 Denis Mahulu, alisema kuwa tamasha hilo linatarajiwa kufanyika kwa siku tatu kuanzia Oktoba 3 hadi 5, mwaka huu, ambapo alisema linaenda sambamba na Siku ya Kahawa Duniani ambayo huadhimishwa Oktoba Mosi ya kila mwaka.
“Wakati wa tamasha hili pia kutakuwa na utoaji wa elimu kuhusiana na faida za kahawa kiuchumi, faida zake kwa wanywaji pamoja na uwepo wa sheria mpya ya utunzaji wa mazingira wakati wa kutekeleza kilimo cha kahawa”, alisema.












