KORONGONI-MOSHI.
Mgombea udiwani wa Kata ya Korongoni kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Issa Elias Juma, amezindua rasmi kampeni yake kwa kishindo huku akiahidi kuwa mtumishi mwaminifu wa wananchi wa kata ya korongoni iwapo atapewa ridhaa ya kuendelea kuwatumikia.
Katika hotuba yake mbele ya mamia ya wakazi wa kata hiyo, Diwani Issa Elias alieleza dhamira yake ya dhati ya kutatua changamoto zinazowakabili wananchi, akitaja vipaumbele mbalimbali vya maendeleo anavyokusudia kuvisimamia.
“Mnanituma kazi, nami ninajituma kutafsiri changamoto zenu kuwa fursa, naahidi kuwa mtumishi wenu mtiifu,” alisema Issa Elias huku akishangiliwa na wananchi waliohudhuria.
Miongoni mwa ahadi alizozitoa ni; kukamilisha ujenzi wa ukuta wa zahanati ya Korongoni, kuboresha miundombinu na mazingira ya Shule ya Msingi Korongoni, kuboresha ajira kwa vijana kwa kutafuta ufadhili wa taa za barabarani kama sehemu ya kukuza biashara ndogondogo
Ahadi zingine ni kwenda kusimamia upatikanaji wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewq na halmashauri kwa vijana, wanawake na walemavu, kuwezesha vijana kupitia taasisi kama SIDO na VETA kwa kuwapa maarifa na uzoefu wa ajira.
Akimnadi diwani huyo, Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini Alhaji Mohamed Shayo, huku akimnadi pia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuwasihi wananchi kumchagua kwa kura zote.
“Twendeni tukampe mama (Rais) kura zote. Tunahitaji maendeleo, kazi ya Mbunge ni kuwa karibu na waliompa kura, kuwasikiliza na kuwahudumia,” alisema Shayo.
Mbunge huyo aliahidi kushirikiana na Diwani kuweka gari la wagonjwa (ambulance) katika zahanati ya Korongoni, sambamba na kutoa usaidizi kwa jamii kupitia magari ya ofisi yake, yakiwemo mabasi kwa ajili ya misiba, harusi, na shughuli nyingine za kijamii.
Vilevile alieleza mikakati ya muda mrefu ya kufufua viwanda, hasa kiwanda cha kusindika ngozi, kwa lengo la kuongeza ajira kwa vijana wa Moshi.
Alisisitiza pia umuhimu wa kuboresha elimu, ujenzi wa kituo cha mabasi cha Moshi, na ushawishi kwa serikali kuweka taa za kuongozea magari maeneo ya hatari kama Mbuyuni.









