MOSHI-KILIMANJARO.
Mbunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki na mgombea ubunge wa Jimbo la Mwanga kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Ngwaru Jumanne Maghembe;
Aliwataka Watanzania kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kwa kumpigia kura mgombea urais wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan, ili aendelee na juhudi za kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli.
Dk. Ngwaru alitoa wito huo jana, wakati wa uzinduzi rasmi wa kampeni za uchaguzi za CCM mkoa wa Kilimanjaro, uliofanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi Nelson Mandela, eneo la Pasua, Manispaa ya Moshi.
Akihutubia maelfu ya wakazi waliojitokeza, Dk. Ngwaru alisema uongozi wa Dk. Samia umeleta mabadiliko makubwa kwenye sekta ya afya, hususan huduma kwa akina mama wajawazito ambao zamani walilazimika kusafiri umbali mrefu kupata huduma bora.
“Zamani mama mjamzito alikuwa anakwenda kujifungua, tunangojea kudra za Mwenyezi Mungu, leo hii, Rais Samia ameleta vifaa tiba vya kisasa; mama mjamzito akifika hospitalini, anapimwa na anajua mtoto amekaa vipi tumboni hata akiwa na ujauzito wa miezi miwili,” alisema Dk. Ngwaru.
Dk. Ngwaru ambaye pia ni mgombea ubunge wa Jimbo la Mwanga, alieleza kuwa serikali ya CCM chini ya uongozi wa Dk. Samia imewezesha upatikanaji wa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika wilaya hiyo.
"Katika kipindi cha miaka minne tu ya Rais Samia, wilaya ya Mwanga imepokea zaidi ya shilingi bilioni 100 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo,” alisema.
Alibainisha kuwa miradi hiyo inahusisha ujenzi wa vituo vya afya, zahanati, hospitali mpya ya wilaya, shule za msingi na sekondari, jengo la utawala, mahakama ya wilaya, stendi ya mabasi pamoja na barabara ya CD Msuya.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, ambaye pia ni mgombea ubunge wa Jimbo la Rombo, alisema sababu za kumchagua Dk. Samia ni nyingi, lakini kubwa zaidi ni kuwa yeye ni kiongozi wa vitendo, si wa maneno.
"Kwa miaka mingi tumekuwa tukisema ‘Kilimo ni uti wa mgongo’, ‘Siasa ni Kilimo’, ‘Kilimo cha kufa na kupona’, lakini bajeti kwenye sekta hii haikuongezwa kama inavyostahili, Dk. Samia amebadilisha hilo,” alisema Prof. Mkenda.
Alieleza kuwa bajeti ya sekta ya kilimo ilikuwa shilingi bilioni 294, lakini chini ya uongozi wa Dk. Samia imeongezeka na kufikia trilioni 1, jambo ambalo ni la kihistoria kwa Wizara hiyo.
Kuhusu sekta ya elimu, Prof. Mkenda alisema serikali imeanza ujenzi wa shule 100 za amali (ufundi), ikiwa ni sehemu ya mageuzi makubwa katika mfumo wa elimu ambapo kila wilaya nchini itakuwa na shule ya ufundi.
“Ifikapo mwaka 2027, mtoto hataishia darasa la saba, elimu ya msingi itakuwa ya miaka 10 hadi kidato cha nne, ili kuwapa wanafunzi ujuzi wa kujiendeleza au kuingia katika soko la ajira,” alifafanua Prof. Mkenda.
Kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 zilianza rasmi Agosti 28 na zinatarajiwa kufikia kilele chake Oktoba 28, kabla ya kufanyika kwa upigaji kura Oktoba 29, mwaka huu.












