MOSHI-KILIMANJARO.
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Moshi Mjini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Ibrahim Mohamed Shayo, Septemba 8,2025 amezindua rasmi kampeni zake katika uwanja wa Mandela, Kata ya Bomambuzi, Manispaa ya Moshi, na kuahidi mageuzi makubwa ya kiuchumi na maendeleo endapo atachaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo.
Katika hotuba yake, Shayo alieleza kuwa moja ya changamoto kubwa inayoikumba Moshi ni kudorora kwa sekta ya viwanda, hali inayosababisha kukosekana kwa ajira na mnyororo duni wa thamani wa mazao.
Alitolea mfano wa Wilaya ya Rombo inayozalisha matunda kwa wingi ikiwemo parachichi, maembe na ndizi, lakini hakuna kiwanda hata kimoja cha kuchakata mazao hayo.
"Mkinichagua nitakwenda kutafuta wawekezaji wakubwa kwa kushirikiana na Serikali ili walete viwanda viwili vya kuchakata matunda, hatutaendelea kuuza mazao ghafi wakati tuna uwezo wa kuongeza thamani hapa hapa," alisema Shayo.
Aidha, aligusia umuhimu wa Moshi kama Mji wa Kiitalii unaopokea wageni wengi kutoka ndani na nje ya nchi, lakini ukosefu wa miundombinu bora kama taa za barabarani ni kikwazo kwa wageni na wakazi.
Aliahidi kuweka taa kuanzia eneo la Kanisa la Kristo Mfalme hadi Soko la Mbuyuni, hatua ambayo itaongeza usalama na kuvutia watalii wengi zaidi.
Katika kukabiliana na changamoto ya msongamano wa magari wakati wa jioni, Shayo aliahidi kufanikisha uwekaji wa taa za kuongoza magari katika maeneo ya Mbuyuni na mzunguko wa saa (round about) ili kurahisisha usafiri na kupunguza usumbufu kwa wananchi.
Shayo pia alieleza azma yake ya kuhakikisha mji wa Moshi unapata hadhi ya kuwa jiji, alisema atafanya mashauriano na Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini ili kupatikane eneo la kuongezwa ndani ya Manispaa ya Moshi, hatua ambayo itasaidia kupanua mipaka na kuongeza fursa za maendeleo.
"Haiwezekani watalii wanapoteremka Kilimanjaro waingie katika Manispaa tu, tunataka wanapofika katika mji wa Moshi wanakaribishwa katika Jiji la Moshi, na hilo linawezekana," alisisitiza.
Katika hatua nyingine, mgombea huyo wa ubunge jimbo la Moshi Mjini, aligusia suala la Standi ya mabasi Ngangamfumuni ambayo haijakamilika kwa muda mrefu, aliahidi kushirikiana na Madiwani, Mkurugenzi wa Manispaa pamoja na Mamlaka husika kuhakikisha ujenzi wa standi hiyo unakamilika kwa wakati.
Shayo alihitimisha hotuba yake kwa kuwaomba wananchi wa Moshi Mjini kumpa ridhaa kupitia kura zao, akisema yuko tayari kuwatumikia kwa uadilifu, uwazi na kwa kushirikiana nao katika kila hatua ya maendeleo.













