CCM MOSHI YAMTANGAZA EMANUEL MLAKI (SABUFFER) KUMNADI MGOMBEA UBUNGE JIMBO LA VUNJO

MOSHI-KILIMANJARO.

Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Moshi imemteua rasmi Mjumbe wake, Emanuel Mlaki, kushiriki katika kampeni za kumnadi mgombea wa Ubunge wa Jimbo la Vunjo kwa tiketi ya CCM, Enock Zadock Koola, kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

Akizungumza katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Moshi kilichofanyika Septemba 5, 2025, Katibu wa CCM Wilaya hiyo, Ramadhani Mahanyu, alithibitisha kuwa Mlaki atakuwa sehemu ya timu ya jukwaani, atakayepanda majukwaa mbalimbali kumpigia kampeni mgombea huyo.

"Kampeni za Jimbo la Vunjo zinatarajiwa kuzinduliwa rasmi Septemba 13, 2025, na katika timu ya watoa hamasa kwa wananchi, Emanuel Mlaki, maarufu kwa jina la Sabuffer, atapanda majukwaani kuhakikisha tunapata kura za kutosha kwa Rais, Mbunge na Diwani," alisema Mahanyu.

Aidha, alibainisha kuwa timu hiyo ya kampeni pia itajumuisha wajumbe wengine wa chama wakiwemo viongozi waandamizi, akiwemo Mwenyekiti wa Jumuiya ya umoja wa Wanawake Tanzania Wilaya ya Moshi Ruwaichi Kaale na Benjamin Mandari, ambaye naye atashirikiana na Mlaki kuhakikisha CCM inapata ushindi wa kishindo katika jimbo hilo.

"Lengo letu ni kuhakikisha kuwa kura za Rais, Mbunge na Madiwani hazipotei.tunakwenda kwa nguvu zote kutafuta ushindi mkubwa," aliongeza Mahanyu.

Kikao hicho ni sehemu ya maandalizi ya kimkakati ya chama kuelekea kampeni za uchaguzi, ambapo CCM inasisitiza mshikamano na ushirikiano baina ya viongozi na wanachama katika kuhakikisha ushindi katika ngazi zote.











Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.