MOSHI-KILIMANJARO.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Moshi, kimetoa onyo kali kwa baadhi ya madiwani wanaotajwa kuanza kampeni za chinichini kwa kutoa rushwa kwa lengo la kujipatia nafasi ya kuwa Mwenyekiti au Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri, kabla ya muda rasmi wa mchakato wa uteuzi kufika.
Kauli hiyo ilitolewa Septemba 5,2025 na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Moshi Sirili Mushi, wakati akizungumza na Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilayani humo katika kikao kilichofanyika kwenye viwanja vya CCM.
Alisema kuna taarifa kwamba baadhi ya madiwani wameanza kuwahonga wenzao walioteuliwa kwa lengo la kujihakikishia nafasi hizo.
"Jamani, bado hujapigiwa kura kuwa diwani, lakini tayari unaanza kupita kwa madiwani wenzako walioteuliwa, kugawa pesa na kuomba kura za kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri, huu ni upotoshaji na ni kinyume na taratibu za chama chetu," alisema Mushi.
Mwenyekiti huyo alifichua kuwa baadhi ya madiwani waliopo kwenye kikao hicho walimpigia simu wakimwomba awapendekeze kwa nafasi hizo za uongozi, jambo ambalo alisema halimo katika mamlaka yake.
"Wako baadhi ya madiwani na wako hapa kwenye kikao, wamenipigia simu kuniomba niwapendekeze kuwa wenyeviti wa halmashauri, mamlaka hayo sina na nimewaambia ukweli," aliongeza.
Katika kikao hicho Mushi aliwahakikishia wajumbe kwamba mchakato wa kuteua viongozi wa halmashauri utafanyika kwa haki na kwa kufuata taratibu rasmi za chama, huku akisisitiza kuwa hakuna atakayepata nafasi kwa kutoa rushwa.
"Tutapendekeza majina matatu kutoka kwa walioomba. Kamati ya Siasa ya Wilaya itakaa chini ya mwenyekiti, majina hayo yataenda mkoa na hatimaye Kamati Kuu ya CCM Taifa itafanya uteuzi, usipoteze muda na pesa zako kuhonga hiyo njia haifanyi kazi kama mimi bado ni Mwenyekiti," alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo wa CCM Wilaya alilitahadharisha chama dhidi ya kuanza kugawanyika kwa makundi kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.
"Chama chetu kimejipanga, tunaomba madiwani na viongozi wafuate taratibu, wasiingie kwenye makundi ambayo yatatuharibia chama, wengi ni wageni, subirini wakati wenu ukifika, chama kina utaratibu wake," alisema.
Aidha, alisema kuwa mchakato wa ujenzi wa ofisi ya chama ngazi ya wilaya umekamilika, na kwamba kutakuwa na ushirikiano wa karibu na wabunge pamoja na madiwani watarajiwa, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanalipa kodi ya ardhi na kuzingatia taratibu zote za chama kutoka ngazi ya wilaya hadi taifa.














