MOSHI-KILIMANJARO
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Ummy Hamis Nderiananga, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kumuamini na kumpa nafasi ya kuwa miongoni mwa wabunge wa viti maalum kutoka kundi la watu wenye ulemavu, kupitia ridhaa ya Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.
Nderiananga alitoa shukrani hizo jana, wakati akizungumza kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Moshi, ambapo alipata nafasi ya kuwasalimia wajumbe wa mkutano huo.
Katika hotuba yake, aliwahimiza wajumbe hao kuendelea kukipigania Chama Cha Mapinduzi (CCM), ili kipate ushindi wa kishindo kwa ngazi zote, kuanzia kwa Rais, Wabunge hadi Madiwani katika uchaguzi mkuu ujao.
"Katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia, serikali imeleta fedha nyingi za maendeleo katika kila mkoa, wilaya na hata kata, hakuna kata ambayo haijaguswa na miradi ya maendeleo, hata pale tulipopata majanga ya mafuriko, Rais Samia alikimbilia kutusaidia," alisema Naibu Waziri Nderiananga.
Kwa upande wake, Kamisaa wa CCM Wilaya ya Moshi ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Godfrey Mnzava, aliwaonya watu wanaoeneza maneno ya kushawishi wananchi wasiwachague wagombea waliopitishwa na chama.
"Kama kuna watu wanaota ndoto, ndoto zenu zisiharibu kura za Rais, Wabunge na Madiwani, wapo wanaosema fulani asipite hizo ni ndoto, kura za rais, wabunge na madiwani ndizo zitakazoamua ushindi wa CCM, tutaendelea kushughulika na wale wanaokiuka msimamo wa chama," alisisitiza Mhe. Mnzava.











