MWANGA-KILIMANJARO.
Serikali kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Wilaya ya Mwanga imedhamiria kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa vyumba zaidi ya 2,000 vya madarasa katika shule za msingi, pamoja na matundu 1,326 ya vyoo, ikiwa ni sehemu ya ajenda ya kuinua elimu katika kipindi cha miaka 2025 hadi 2030.
Ahadi hizo zimetolewa kupitia taarifa ya mgombea ubunge wa Jimbo la Mwanga kwa tiketi ya CCM, Dk. Ngwaru Maghembe, ambaye alisema kuwa serikali pia imepanga kujenga shule mpya za msingi nne, shule za kata nne, pamoja na nyumba nane za walimu ili kuimarisha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.
Kwa upande wa elimu ya sekondari, Dk. Maghembe alisema kuwa serikali imepanga kujenga madarasa 85, mabweni 48, na mabwalo 33 katika shule za sekondari katika kipindi hicho cha miaka mitano.
Katika sekta ya miundo mbinu ya barabara, Dk. Maghembe alisema serikali imekwishapata fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Kikweni–Buchama yenye urefu wa kilomita 9 kwa kiwango cha lami, ambayo ni sehemu ya barabara kuu ya km 29.5 inayotarajiwa kukamilishwa kwa kiwango cha juu.
“Barabara hii ina urefu wa kilomita 29.5, lakini sehemu ya kilomita 9 ndiyo iliyokuwa haijakamilika, fedha tayari zimepatikana na serikali ya CCM imejipanga kuikamilisha mwaka huu,” alisema.
Aidha, miradi mingine ya barabara inayotarajiwa kutekelezwa kwa kiwango cha lami ni pamoja na: Kisangara–Shighatini–Usangi–Kwa Hindi, Jipe–Kambi ya Simba, Mgagao–Karamba–Toroha, Kilomeni–Kambi ya Simba na Mlembea–Kivanda–Tangwa.
Dk. Maghembe alisema utekelezaji wa miradi hiyo ni sehemu ya dhamira ya CCM kuhakikisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii yanawafikia wananchi wa Mwanga kwa usawa na haraka zaidi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilayani humo Ibrahim Mnzava, aliwashukuru wananchi wa Usangi kwa kuhudhuria kwa wingi kwenye mkutano huo wa kampeni huku akiwaomba na siku ya kupiga kura Oktoba 29 mwaka huku akiwaomba wananchi kuwapigia kura ya ndio wagombea wote wanaotokana na Chama cha Mapinduzi CCM.







