CONCEPT ONE FOUNDATION KUPELEKA ELIMU YA MAZINGIRA MASHULENI

MOSHI-KILIMANJARO.

Katika juhudi za kulinda na kuhifadhi mazingira kupitia elimu, Shirika lisilo la Kiserikali la Concept One Foundation limezindua mpango mkakati wa kupeleka elimu ya mazingira mashuleni, ambapo wanafunzi watatumia vifaa vya kisasa vya kidijitali (tablets) katika kujifunza masuala yanayohusu mazingira.

Ernest Dominic, ambaye ni Mtaalamu wa Jiografia ya Mazingira kutoka shirika hilo, alisema lengo ni kuwajengea wanafunzi uwezo wa kufikiri kwa kina, kupambanua hoja, na kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto za kimazingira.

"Hatulengi kutumia tu elimu ya nadharia kama ilivyokuwa zamani, bali tunatamani mtoto anapojifunza aweze kuelewa kwa kina na kuishi na maarifa hayo kichwani,” alisema Dominic.

Alieleza kuwa shirika hilo linatarajia kuanza utekelezaji wa mpango huo mwishoni mwa mwezi Septemba mwaka huu, likianzia na kata ya Uru Kusini kwa wanafunzi wa darasa la nne hadi darasa la sita.

Mbali na kutumia vifaa vya kidijitali katika ufundishaji, mpango huo pia unalenga kuwajengea watoto uelewa wa umuhimu wa kutunza mazingira ili wawe mabalozi wa mabadiliko chanya hata katika familia zao.

“Leo hii mzazi anapoharibu mazingira, mtoto anaogopa kumkosoa kwa hofu ya kupigwa. Tunapowapa watoto elimu ya mazingira, wanapata ujasiri na uelewa wa kumwambia mzazi wake, ‘unachofanya si sahihi,’” aliongeza.

Katika warsha iliyowakutanisha walimu wakuu wa shule za msingi, walimu wa mazingira, viongozi wa vijiji na maafisa elimu, Dominic alisema upandaji miti katika shule ni sehemu muhimu ya mazingira bora ya kujifunzia.

“Miti inatoa kivuli kwa watoto wakati wa jua kali, lakini pia huwasaidia kujisomea katika mazingira ya nje kwa utulivu,” alisema.

Kwa upande wake Afisa Elimu Watu Wazima kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Robert Kasumbai, alisema halmashauri hiyo ina jumla ya shule za msingi 271 na shule za sekondari 104, na kutoa wito kwa Concept One Foundation kupanua wigo wake kufikia shule nyingi zaidi.

Adria Laswai, Mkuu wa Shule ya Msingi Longuo, alisema ujio wa vifaa hivyo vya kidijitali utakuwa kichocheo kikubwa kwa wanafunzi kuongeza ari ya kujifunza.

"Watoto watapata zana mbalimbali za kiteknolojia zitakazowasaidia kuelewa masuala ya mazingira kwa urahisi na kwa njia ya kisasa,” alisema Laswai.

Naye Salum Hamad Mvano kutoka Concept One Foundation, alisema upandaji miti ni hatua muhimu katika kuhifadhi mazingira, ikiwa ni pamoja na kulinda vyanzo vya maji, kuzuia mmomonyoko wa ardhi na kuimarisha mfumo wa maji ya chini kwa chini.

“Katika mwaka wa 2022/2023, tuliweza kupanda miti katika maeneo mbalimbali ikiwemo Ronga miti 400, Bonite 980, Weruweru 700, Miwaleni 1,380, Katanini 1,310 na Kitopeni miti 5,230,” alisema Mvano.

Mpango huu wa shirika la Concept One Foundation unaonekana kuwa hatua ya kimkakati na ya mfano katika kuunganisha teknolojia, elimu na utunzaji wa mazingira kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.



Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.