MWANGA-KILIMANJARO.
Mgombea ubunge mteule wa Jimbo la Mwanga kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Ngwaru Jumanne Maghembe, ameipongeza Serikali inayoongozwa na mgombea urais wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa fedha zilizowezesha kufufuliwa na kukamilika kwa mradi mkubwa wa maji wa Mwanga–Same–Korogwe, ambao kwa sasa umewapatia wakazi wa Mwanga huduma ya maji safi na salama.
Dk. Ngwaru alitoa pongezi hizo jana katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kata ya Usangi, ambapo aliwahutubia wakazi waliojitokeza kwa wingi kumsikiliza.
"Mimi nimekuwa Mbunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa miaka minane. Nchi yetu ni ya kipekee ndani ya Jumuiya, tuna bahati kubwa kuishi kwa amani, uhuru na kuwa na mipango mizuri ya maendeleo,” alisema.
Aliendelea kusisitiza kuwa mafanikio hayo yanatokana na uongozi makini wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ambaye ni mfuatiliaji mzuri wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
"Mradi wa Mwanga–Same–Korogwe ulianza mwaka 2014 lakini ulisuasua, ni hadi pale Rais Samia alipoamua kutoa fedha ndipo mradi ukaendelea na sasa umekamilika, hili linaonyesha jinsi tulivyo na viongozi wachapa kazi,” alisema Dk. Ngwaru.
Katika sekta ya afya, Dk. Ngwaru alisema serikali inayoongozwa na CCM itajenga vituo vya afya na zahanati kwenye maeneo yenye uhitaji mkubwa, huki alitangaza mpango wake wa kusaidia kila zahanati mpya kwa kutoa tofari 5,000 na mifuko 100 ya saruji ili kuharakisha ujenzi na kupunguza mzigo kwa wananchi.
Alibainisha kuwa serikali tayari imejenga majengo 10 katika Hospitali mpya ya Wilaya ya Mwanga, na majengo 18 mengine yanapangwa kujengwa, ikiwemo chumba cha upasuaji na jengo la huduma ya mama na mtoto katika Kituo cha Afya Chomvu.
Akizungumzia miundo mbinu, Dk. Ngwaru alisema serikali imepanga kujenga baadhi ya barabara kwa kiwango cha lami ili kuwezesha shughuli za uzalishaji mali.
Alisema pia serikali itakarabati minada ya ng’ombe ya Kileo na Mgagao, kwa lengo la kuifanya kuwa kitovu cha biashara ya mifugo kwa Kanda ya Kaskazini.
Aidha, aliahidi kushughulikia changamoto ya umeme katika vitongoji sita ambavyo bado havijafikiwa na huduma hiyo.
Katika sekta ya kilimo, Dk. Ngwaru aliahidi kusimamia ukarabati na uboreshaji wa miundombinu ya umwagiliaji pamoja na ujenzi wa soko la mazao la Kituli.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mwanga, Ibrahim Mnzava, aliwataka wananchi kuchagua wagombea makini wa CCM katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, mwaka huu.
"Tusiwachague wagombea wa upinzani ambao hawana sera wala ilani ya utekelezaji, tuchague Dk. Samia Suluhu Hassan kwa urais, Dk. Ngwaru Maghembe kwa ubunge na madiwani wote wa CCM,” alisema.









