ALIYEKUWA MGOMBEA UDIWANI WA CHAUMA KATA YA CHOMVU, HALIFA HASSANI ISAE, ATANGAZA KUREJEA CCM

MWANGA-KILIMANJAO.

Aliyekuwa mgombea wa nafasi ya Udiwani kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMA) katika Kata ya Chomvu, Halifa Hassani Isae, ametangaza rasmi kurejea katika Chama Cha Mapinduzi (CCM), akieleza dhamira yake ya kushirikiana na viongozi wa chama hicho kuwatumikia wananchi kwa maslahi ya pamoja.

Isae alitoa tamko hilo mbele ya mamia ya wakazi wa Usangi katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni za CCM uliofanyika kwenye viwanja vya VTC Usangi, Agosti 29,2025.

Akihutubia wananchi, Isae alitoa wito kwa wanachama na wafuasi wa CCM kumuunga mkono Mbunge wa Jimbo la Mwanga, Dk. Ngwaru Jumanne Maghembe, kwa kusema:

"Ninawaomba wana CCM, tumepata mbunge Dkt. Ngwaru Jumanne Maghembe, nawaombeni tumuunge mkono. Nawaomba tusipeleke shida zetu binafsi kwake; twendeni tupeleke shida za wananchi."

Alisisitiza kuwa ni muhimu kujenga hoja zinazohusu maendeleo ya jamii kwa ujumla badala ya matatizo ya mtu mmoja mmoja:

"Kwani mtu akipeleka shida zake binafsi, hataweza kutatua changamoto za kila mtu mmoja mmoja, tunatakiwa tujenge hoja za miradi ambayo tukimpelekea mbunge, ataweza kuisemea bungeni na hatimaye miradi hiyo itufikie sote, ili kila mtu aweze kunufaika, si mtu binafsi."

Isae pia aliwaonya wananchi dhidi ya tabia ya kwenda kwa wabunge kutafuta msaada wa matatizo ya nyumbani:

"Acheni kumwendea mbunge akusaidie changamoto za nyumbani kwako hiyo haitafaa twendeni kwa mbunge na madiwani kuwaeleza changamoto za kata zetu au za kijimbo."

Akieleza sababu ya kurejea CCM, Isae alisema: "Mimi niligombea Kata ya Chomvu kupitia CHAUMA nikitarajia kwamba wangenichagua wananchi ili niweze kuwasemea, lakini haikuwezekana hivyo nimeamua kurudi CCM ili niweze kuungana na mbunge katika kumsemea mazuri ya CCM."

Hatua ya Isae kurejea CCM imepokelewa kwa hisia mbalimbali, huku baadhi ya wachambuzi wa siasa wakitafsiri hatua hiyo kama kuimarika kwa mvuto wa CCM katika Jimbo la Mwanga kuelekea uchaguzi ujao.










Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.