MWANGA-KILIMANJARO.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mwanga kimempongeza aliyekuwa mgombea wa nafasi ya ubunge kupitia chama hicho, Alpha Zidiheri Mshana, kwa uamuzi wake wa kumuunga mkono mgombea mteule wa CCM, Dk. Ngwaru Jumanne Maghembe, licha ya kutokupata nafasi kupitia kura za maoni.
Pongezi hizo zilitolewa Agosti 30, 2025, na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mwanga, Ibrahim Mnzava, wakati wa uzinduzi rasmi wa kampeni za chama hicho uliofanyika kwenye uwanja wa VTC, Usangi.
Mnzava alisema kuwa katika mchakato wa kura za maoni uliohusisha watia nia 28, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM ilirejesha majina manane kwa ajili ya kuchujwa zaidi, na kwamba ni Alpha Zidiheri Mshana pekee aliyejitokeza hadharani kumuunga mkono mshindi wa mchakato huo, Dk. Maghembe.
"Tunaendelea kusisitiza umoja ndani ya chama. Uamuzi wa Mshana ni wa kuigwa na ni mfano wa uaminifu na uzalendo wa kweli kwa CCM, anapaswa kupongezwa," alisema Mnzava.
Kwa upande wake, Alpha Zidiheri Mshana alieleza kuwa anajivunia kushiriki mchakato wa ndani ya chama kwa njia ya haki na amani, na kwamba licha ya kushika nafasi ya nne kwa kupata kura 98, ataendelea kuwa bega kwa bega na mgombea mteule katika kampeni zote.
"Katika mchakato wa kura za maoni, Dk. Ngwaru Maghembe alipata kura 4,108, Joseph Tadayo kura 1,689, Ramadhani Ally Mahuna kura 720, na mimi nikiwa wa nne kwa kura 98. Nimeamua kwa hiari yangu kuungana na Dk. Maghembe kwa ajili ya kuhakikisha CCM inashinda kwa kishindo," alisema Mshana.
Alisema atashiriki kikamilifu katika kampeni za CCM jimboni Mwanga na kutoa wito kwa wanachama wengine kuweka mbele maslahi ya chama kuliko ya mtu binafsi.
"Kampeni si uhasama, ni majadiliano ya sera na mipango ya maendeleo, niko tayari kutumia nguvu zangu zote kumuunga mkono mgombea wetu mteule hadi ushindi upatikane," aliongeza.
Kwa ujumla, tukio hilo limepongezwa na wanachama wengi wa CCM kama ishara ya mshikamano na utulivu ndani ya chama, hasa katika kipindi muhimu cha kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.











