DK. MAGHEMBE: SITAKUBALI TEMBO WAENDELEE KUTAWALA MAISHA YA WANANCHI MWANGA

MWANGA-KILIMANJARO.

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Mwanga mkoani Kilimanjaro kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Ngwaru Jumanne Maghembe, amesema kuwa hatokubali kuona wananchi wa jimbo hilo wakiendelea kuteseka kwa sababu ya uvamizi wa wanyamapori, hasa tembo, na kwamba atalipa kipaumbele cha kwanza tatizo hilo pindi atakapochaguliwa kuwa Mbunge.

Dk. Maghembe alitoa kauli hiyo  Agosti30,2025, katika uzinduzi wa kampeni za CCM kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu, uliofanyika kwenye uwanja wa VTC, Usangi, wilayani humo.

Alisema kuwa uvamizi wa tembo umekuwa kero kubwa kwa wananchi katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo zikiwemo tarafa za Jipendea, Kwakoa, Mgagao, Kirya, Kivisina na Toroha na kwamba kuna haja ya kuweka mfumo rasmi wa usimamizi na ufuatiliaji wa changamoto hiyo.

“Nitashirikiana na mamlaka husika kuhakikisha TAWA inafungua ofisi yake wilayani Mwanga, ili kuwe na maofisa wa taasisi hiyo karibu na wananchi, tofauti na hali ya sasa ambapo wanalazimika kusubiri maofisa kutoka wilaya jirani ya Same,” alisema Dk. Maghembe.

Kuhusu fidia kwa waathirika wa uvamizi wa wanyamapori, alisema kuwa atahakikisha anafuatilia suala hilo mapema iwezekanavyo, kwani taarifa zinaonyesha kuwa mara ya mwisho fidia hiyo ilitolewa mwaka 2022.

Mbali na changamoto ya wanyamapori, Dk. Maghembe alibainisha vipaumbele vingine ambavyo atavifanyia kazi ikiwa ni pamoja na huduma ya mawasiliano katika kata za Msangeni, Kivisini, Mwaniko, Chomvu, Ngujini na Kirya, ambazo kwa sasa bado zinakabiliwa na tatizo la mtandao hafifu.

Alisema pia kuwa upatikanaji wa maji safi na salama katika Tarafa ya Ugweno utakuwa kipaumbele kingine, akieleza kuwa afya ya jamii haiwezi kutenganishwa na huduma hiyo muhimu.

“Kwa mtu kuwa na afya njema ni pamoja na kuwa na uhakika wa kupata maji safi na salama; hili nitalipa msisitizo na kulifanyia kazi kwa haraka,” alisisitiza.

Kuhusu sekta ya nishati, aliahidi kufuatilia kwa karibu kuhakikisha vitongoji sita ambavyo bado havijafikiwa na huduma ya umeme vinapatiwa huduma hiyo ndani ya muda uliopangwa.

Katika kukabiliana na tatizo la ajira kwa vijana, Dk. Maghembe alisema atashirikiana na mamlaka husika kuhakikisha elimu ya ujasiriamali inatolewa kwa vijana, na mikopo ya halmashauri kwa makundi maalum inaboreshwa na kutolewa kwa wakati ili kuwawezesha kujiajiri.

Aliongeza kuwa ataweka mkazo katika kuboresha minada ya mifugo ya Kileo na Mgagao, ili iweze kutumika kama fursa za kiuchumi kwa vijana na wafugaji wa jimbo hilo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mwanga, Ibrahim Mnzava, aliwataka wananchi kuwaamini wagombea wa CCM katika nafasi zote, akisisitiza kuwa Ilani ya chama hicho inalenga kuboresha maisha ya Watanzania na kukuza uchumi wa Taifa.

“Mamlaka zetu zimefanya kazi kubwa kutuletea wagombea wa uhakika, hivyo ni jukumu letu sasa kuwachagua ili kazi nzuri iliyofanywa chini ya Rais Samia Suluhu Hassan iendelee,” alisema Mnzava.



















Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.