MOSHI – KILIMANJARO.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, amemkabidhi cheti cha pongezi binti aliyewahi kuhukumiwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa, ikiwa ni ishara ya kutambua mabadiliko makubwa aliyoyafanya katika maisha yake baada ya kutoka gerezani.
Tukio hilo lilifanyika Agosti 26, 2025, wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 64 ya Jeshi la Magereza yaliyofanyika katika viwanja vya Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania (TCTA), Ukonga – Dar es Salaam.
Waziri Mkuu Majaliwa alieleza kuwa serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa waliokuwa wafungwa, hasa wale wanaojitahidi kubadilika na kuwa raia wema.
Aliwataka Watanzania kuacha tabia ya kuwanyanyapaa waliowahi kuwa magerezani, bali wawape nafasi ya kuanza maisha mapya na kuchangia maendeleo ya taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari Agosti 28, 2025 ofisini kwake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Tanzania Ex-Prisoners Foundation (TEPF), Rose Malle, alithibitisha kupokea cheti hicho kwa niaba ya taasisi yake, ambayo imekuwa ikihudumia wafungwa waliomaliza vifungo kwa kuwawezesha kielimu na kiuchumi.
"Adhabu ya kifungo ni sehemu ya maisha ambayo si vyema mtu akairudia, mtu anapopata fursa ya kutoka gerezani hana budi kujirekebisha na kuishi kwa kufuata maadili mema," alisema Malle.
Alibainisha kuwa cheti hicho kilitolewa na Idara ya Magereza nchini kama kutambua mchango wa TEPF katika kuwasaidia waliomaliza vifungo kurudi kwenye maisha bora yenye maadili.
“Tuzo hii imetupa hamasa kubwa. Inadhihirisha kuwa kazi tunayoifanya inatambulika na kuthaminiwa na serikali kupitia Jeshi la Magereza,” aliongeza.
Katika mahojiano hayo, Malle alisimulia kwa masikitiko jinsi alivyoshtakiwa mwaka 2012 kwa kosa la mauaji ya dereva wa bodaboda, ambapo baada ya kesi kudumu kwa miaka minne, alihukumiwa kunyongwa mwaka 2015 akiwa na umri wa miaka 21.
Alieleza kuwa wakati wa tukio, alikuwa na umri wa miaka 18 na alikamatwa kwa kosa ambalo baadaye ilibainika halikuwa la kwake. “Baada ya kuhukumiwa, nilikata rufaa katika Mahakama ya Rufani Arusha, na mwaka 2017 nilishinda rufaa hiyo na kuachiwa huru,” alisema kwa hisia kali huku akibubujikwa na machozi.
Alisema kuwa mkutano na Waziri Mkuu, ambaye alihusika pia kwa namna moja au nyingine katika kufanikisha kuachiwa kwake, ulikuwa wa faraja kubwa kwake binafsi.
Akizungumzia shughuli za TEPF, Malle alisema taasisi hiyo huwapa elimu ya ujasiriamali na ufundi wafungwa waliomaliza vifungo ili waweze kujitegemea na kujenga maisha mapya wakiwa uraiani.
Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa Magereza, Jeremiah Katungu, alisema jamii ina jukumu la kuwapokea waliomaliza vifungo na kushirikiana na Jeshi la Magereza katika kuendeleza kazi ya urekebishaji.
“Maadhimisho haya ni fursa ya kujitathmini, kujifunza tulikotoka na kujipanga kwa mustakabali bora wa huduma za urekebishaji,” alisema Katungu.
Maadhimisho ya mwaka huu yaliendeshwa chini ya Kauli mbiu: "Ushirikiano wa Jeshi la Magereza na Jamii kwa Urekebishaji Wenye Tija."
Naye mmoja wa wanufaika wa mpango wa Parole, Rachael Reko, alieleza jinsi alivyopata ujuzi wa kushona na mapishi akiwa gerezani, jambo lililomsaidia kuanza maisha mapya kwa matumaini baada ya kumaliza kifungo chake cha miaka minne kwa kosa la kujeruhi.





.webp)


.webp)





