MOSHI-KILIMANJAO.
Wito umetolewa kwa wale wanaomaliza adhabu ya vifungo vya Magereza kuepuka vitendo ambayo vitafanya warudie vifungo vyao au adhabu nyingine kubwa zaidi.
Rai hiyo imetolewa Agosti 28,2025 na Mkurugenzi wa taasisi ya kuhudumia wafungwa waliomaliza muda wao wa vifungo magarezani ya Tanzania Ex-Prisoners Foundation (TEPF) Rose Malle, wakati akiongea na Waandishi wa Habari kuhusiana na cheti cha pongezi ilichopata taasisi hiyo hivi karibuni, kutokana na shughuli inazofanya.
“Adhabu ya kifungo ni sehemu ya maisha ambayo si vyema mtu akairudia badala yake mtu anapopata fursa ya kutoka kifungoni aidha kwa kumaliza muda wake wa kifungo au kwa sababu nyingine yoyote hana budi kurudia maadili mema na kuepuka kurudi huko”, alisema.
Akizungumzia cheti hicho, Malle alisema kuwa kilitolewa na Idara ya Magereza nchini katika kutambua mchango wa taasisi hiyo katika kuwasaidia wafungwa waliomaliza muda wao magerezani ili warudi kwenye maisha ya zamani yenye maadili mema.
“Tulikabidhiwa cheti hiki na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Agosti 26, mwaka huu, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 64 tangu kuanzishwa kwa taasisi ya Magereza hapa nchini”, alisema.
Aliongeza, “Tuzo hii imetutia moyo sana; imetupa ari ya kufanya vizuri zaidi kwa vile shughuli zetu zinatambulikana na kuthaminiwa na serikali kupitia Idara yake ya Magereza hapa nchini”.
Malle aliendelea kusema kuwa mbali na kupokea cheti hicho, pia tukio limempa faraja ya kipekee kwa kumkutanisha na Waziri Mkuu ambaye yeye (Waziri Mkuu) alifanikisha kuachiliwa kwake (Malle) kutoka gerezani alipokuwa akingojea hukumu ya kifo, kabla ya kutoka na kuanzisha taasisi hiyo.
Akizungumzia shughuli zinazofanywa na taasisi hiyo, Malle alisema ni pamoja kuwapa elimu wafungwa waliomaliza muda wao ili waweze kufanya shughuli zitakazowawezesha kujikimu na kuendelea na maisha baada ya adhabu walizotumikia.
“Elimu hizo ni pamoja na ujasiriamali, sambamba na ile ya ufundi; elimu wanazopata zitawawezesha kupata ajira na hata kujiajiri wenyewe na hivyo kuweza kujikimu wao na wanafamilia wao kwa wale wenye familia”, alisema.


