SERIKALI YARUHUSU UWEKEZAJI WA BUSTANI ZA WANYAMAPORI KWENYE HIFADHI ZA MISITU

MOSHI-KILIMANJARO.

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imesema Serikali imeruhusu uwekezaji wa bustani za wanyamapori katika hifadhi zake za misitu, hususan zile zilizo karibu na miji, ikiwa ni mkakati wa kuongeza hamasa ya utalii wa ndani.

Hayo yalisemwa jana na Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Prof. Dos Santos Silayo, wakati wa kilele cha Kampeni ya TUKACHARU RAU FOREST CHARITY TOUR–Msimu wa Tatu, iliyofanyika ndani ya Hifadhi ya Mazingira Asilia Rau, uliopo mjini Moshi, mkoa wa Kilimanjaro.

Akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi TFS, Mhifadhi Mwandamizi wa TFS Yusuph Tango, alisema kuwa Serikali kupitia kanuni za uhifadhi, imeamua kufungua milango kwa wawekezaji kuanzisha bustani za wanyamapori katika baadhi ya hifadhi za misitu ili kuwavutia watalii na kuleta maendeleo katika sekta ya uhifadhi na utalii wa asili.

“Nitoe wito kwa wawekezaji na wadau mbalimbali kufika katika ofisi zetu. Watashauriwa na wataalamu wetu wa uhifadhi na kuonyeshwa fursa zilizopo katika hifadhi zetu, zikiwemo maeneo yanayofaa kwa bustani za wanyamapori,” alisema Tango.

Alibainisha kuwa bustani hizo zitakuwa sehemu ya vivutio vya utalii wa kielimu, hasa kwa watoto na wageni wa ndani na nje, watakaokuja kujifunza kuhusu miti na wanyamapori katika mazingira halisi ya misitu ya asili.

“Natoa rai kwa wadau wa sekta ya utalii, hususan makampuni ya ndani ya Wilaya ya Moshi, kuendelea kushirikiana nasi katika kukuza utalii wa ndani na kuwaleta watalii kutembelea hifadhi ya mazingira asilia Rau,” aliongeza.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, aliwataka wadau wa sekta ya utalii kuchangamkia fursa hiyo muhimu kwa kuwekeza katika bustani hizo huku akihimiza wageni wa ndani na nje ya nchi kuendelea kutembelea hifadhi ya mazingira asilia Rau.

“Msitu huu wa Rau ni hazina kubwa kwa maendeleo ya utalii wetu, fursa hii ya uwekezaji ni ya kipekee, na ni wajibu wetu kushirikiana kuiendeleza,” alisema Mnzava.

Tamasha hilo liliambatana na hitimisho la Kampeni ya TUKACHARU RAU FOREST CHARITY TOUR, iliyoandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Wialaya ya Moshi kwa ushirikiano na TFS-Moshi kwa lengo la kutoa misaada kwa makundi ya watu wasiojiweza sambamba na kuwapa fursa washiriki kutalii ndani ya msitu huo wa asili.









Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.