MOSHI-KILIMANJARO.
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Vunjo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Enock Zadock Koola, mnamo Agosti 26, 2025, amechukua fomu ya uteuzi katika Ofisi ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa ajili ya kuwania nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.
Akizungumza na mamia ya wananchi waliomsindikiza katika zoezi hilo, Koola aliwataka Watanzania, hususan wapiga kura wa Jimbo la Vunjo, kumpa imani na ridhaa Rais Samia Suluhu Hassan ili aweze kuendelea na kazi nzuri alizozianzisha katika kipindi cha uongozi wake.
“Mama Samia amefanya makubwa ndani ya kipindi cha miaka minne tu ya uongozi wake, ikiwemo miradi mingi ya maendeleo hapa Vunjo. Shukrani zetu kwake ni kumpa fursa nyingine kupitia kura zetu ili aendelee na kazi nzuri aliyoianza, kwani katiba inamruhusu,” alisema Koola huku akishangiliwa na wafuasi wake.
Aidha, alieleza kuwa yeye pamoja na wagombea wenzake wa nafasi za ubunge na udiwani kupitia CCM, wako tayari kuwatumikia wananchi kwa weledi, lakini kazi hiyo itakuwa nyepesi zaidi endapo Rais Samia ataendelea kuongoza serikali.
"Tukiongozwa na Mama Samia, tutakuwa na nguvu na dira ya pamoja katika kuwahudumia Watanzania, hii ni serikali inayoleta maendeleo yanayoonekana,” aliongeza.
Koola pia alieleza kuwa zaidi ya Shilingi trilioni 1.4 zimeletwa mkoani Kilimanjaro katika kipindi cha miaka mitatu tu ya uongozi wa awamu ya sita, na kutaja hatua hiyo kuwa ni uthibitisho wa dhamira ya dhati ya Rais Samia kuwaletea maendeleo wananchi.
Katika hatua nyingine, aliwataka wananchi kudumisha mshikamano na umoja katika kipindi chote cha uchaguzi, akisisitiza kuwa utulivu na amani ni misingi muhimu ya kuimarisha maendeleo ya taifa baada ya uchaguzi.









