MOSHI-KILIMANJARO.
Mgombea udiwani wa Kata ya Miembeni, Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, Haruna Ally Mushi, ameahidi kuwa kiungo madhubuti kati ya wananchi na serikali endapo atapewa ridhaa ya kuongoza kata hiyo.
Akizungumza leo Agosti 27, 2025, muda mfupi baada ya kurejesha fomu ya uteuzi kwa Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi wa kata hiyo, Ritha Swai, Mushi alisema uzoefu wake utamsaidia kuwasilisha kero na mahitaji ya wananchi kwa mamlaka husika kwa ufanisi.
“Kwa uzoefu wangu, nitakuwa daraja kati ya wananchi na serikali katika shughuli za maendeleo, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha miradi inayoendelea kutekelezwa inakamilika kwa manufaa ya wananchi,” alisema Mushi.
Aidha, alibainisha kuwa atashirikiana na viongozi wengine akiwemo mbunge atakayechaguliwa, kuhakikisha utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) unafanyika kwa ufanisi chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
“Kuelekea Uchaguzi Mkuu, CCM itawaahidi wananchi maendeleo kupitia ilani yake. Nitashirikiana na viongozi wenzangu kuhakikisha ahadi hizo zinatekelezwa ipasavyo endapo tutapewa ridhaa ya kuongoza,” aliongeza.
Kwa upande wake, Katibu wa CCM wa Kata ya Miembeni, Agnes Kambi, aliwataka makatibu wa Jumuiya kuhakikisha ushindi wa chama hicho kwa kuhakikisha upatikanaji wa kura nyingi kwa Rais, Mbunge na Diwani.
“Makatibu wa Jumuiya, tunapeana majukumu kwa ajili ya kuhakikisha ushindi wa CCM. Kuanzia tunapotoka hapa kurejesha fomu ya mgombea wetu, Haruna Ally Mushi, tunakwenda kukutana na makundi yetu ya kampeni ili kuhakikisha kazi ya kutafuta ushindi inafanyika kikamilifu,” alisema.
Kambi aliongeza kuwa ni muhimu kwa wanachama kuhamasisha kampeni za nyumba kwa nyumba kupitia jumuiya zao ili kufanikisha ushindi wa chama katika uchaguzi ujao.













