MWANGA-KILIMANJARO.
Mbunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki na mgombea Ubunge wa Jimbo la Mwanga kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Ngwaru Jumanne Maghembe, ameahidi kuendeleza pale walipoishia watangulizi wake, akiahidi kuleta maendeleo endelevu kwa wananchi wa Mwanga.
Dkt. Ngwaru alitoa kauli hiyo Agositi 26,2025 muda mfupi baada ya kuchukua fomu ya uteuzi kutoka kwa Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo hilo Richard Tarimo, hafla iliyofanyika Wilayani Mwanga, mkoani Kilimanjaro.
Akizungumza mbele ya umati wa wanachama wa CCM waliofurika nje ya jengo jipya la Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, Dkt. Ngwaru alianza kwa kutoa shukrani za dhati kwa viongozi waliomtangulia, akiwemo Waziri Mkuu Mstaafu na "Baba wa Mwanga", Hayati Cleopa David Msuya, aliyekuwa Mbunge wa kwanza wa jimbo hilo.
Aidha, alimshukuru Profesa Jumanne Maghembe, ambaye pia ni Baba yake mzazi, kwa kulitumikia Jimbo hilo kwa kipindi cha zaidi ya miaka 25 kwa uaminifu, juhudi, na uzalendo mkubwa.
Dkt. Ngwaru pia alitoa heshima kwa mtangulizi wake, Wakili Msomi Joseph Thadayo, kwa uongozi wake na mchango kwa maendeleo ya wananchi wa Mwanga.
Katika hotuba yake, Dkt. Gwaru aliahidi kushughulikia kwa haraka changamoto za msingi zinazolikabili Jimbo hilo, zikiwemo vijiji ambavyo bado havijaunganishwa na huduma ya umeme, pamoja na uhaba wa vyumba vya madarasa katika baadhi ya shule za msingi, pamoja na standi ya mabasi.
“Tutahakikisha kila kijiji kinaunganishwa na nishati ya umeme, na watoto wetu wanasoma katika mazingira rafiki na salama, haya ni mambo ambayo hayapaswi kuwa changamoto tena katika karne hii ya 21,” alisema Dkt. Ngwaru.
Aidha alizungumzia changamoto ya wanyama wakali tembo, ambapo aliwaahidi wananchi wa jimbo hilo, changamoto hiyo atakwenda kushughulika nayo kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii.
Akizungumzia mchakato wa kura za maoni ndani ya chama, Dkt. Ngwaru aliwashukuru wanachama wa CCM kwa imani kubwa waliyoionyesha kwake.
Katika uchaguzi huo wa ndani, Dkt. Ngwaru aliibuka mshindi kwa kupata kura 4,108, akimshinda aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Joseph Anania Thadayo, aliyepata kura 1,689, huku Ramadhani Ally Mahuna akipata kura 720.
Alisisitiza kuwa uchaguzi wa ndani umekamilika kwa amani na demokrasia, na sasa juhudi zote zinaelekezwa kwenye ushindi wa CCM katika uchaguzi mkuu ujao.
“Ni wakati wa kuwa kitu kimoja kama wana-CCM. Tumevuka hatua muhimu, sasa kazi ni kuhakikisha Jimbo la Mwanga linaendelea kubaki imara chini ya CCM, kwa ushindi wa kishindo,” alihitimisha Dkt. Ngwaru kwa kauli ya matumaini.











