Vyama tisa vya siasa vyenye usajili wa kudumu kati ya 18,vimechukua fomu kuwania
kiti cha ubunge jimbo la moshi mjini katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika
mwezi oktoba mwaka huu.
Vyama hivyo ni Chama cha Mapinduzi (CCM), Chama cha
wananchi (CUF), CCK, NRA, TLP, MAKINI, SAU, AAFP na Chama cha CHAUMA.
Msimamizi wa
uchaguzi Jimbo la Moshi mjini Sifael Kulanga, aliyasema hayo Agosti 25,2025 wakati wa zoezi la uchukuaji na
urejeshaji wa fomu likitarajiwa kuhitimishwa Agosti 27 saa kumi jioni.
Mgombea Ubunge Jimbo la Moshi mjini kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Ibrahim Shayo maarufu kwa
jina la (Ibra Line) ni miongoni mwa wagombea waliochukua fomu kwenye Tume hiyo.
Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu, Shayo alisema anakishukuru chama chake
kwa kumwamini na kumteua kupeperusha bendera ya chama hicho.
"Hakuna siku
nimekuwa na furaha kama ya leo, namshukuru sana Mwenyekiti wangu wa CCM Taifa na Kamati yake kwa kuniteua kugombea nafasi hii, niko tayari kushirikiana na
wana Moshi kuhakikisha chama kinapata ushindi",alisema.
Alisema kazi iliyopo yake
kwa sasa ni kwenda kushirikiana na viongozi wa chama hicho ili kushinda Uchaguzi Mkuu na kuwaletea
maendeleo wananchi wa Moshi.
Shayo, alisisitiza ushirikiano kutoka kwa makada wenzake
waliojitokeza kuomba ridhaa ya chama hicho kuwania kiti hicho lakini kura
hazikutosha.
Aidha alitangaza kuvunjwa kwa makundi yote na kuelekeza nguvu ya pamoja
kuhakikisha jimbo hilo linaendelea kuwa mikononi mwa chama cha Mapinduzi.
Katika
zoezi hilo la uchukuaji wa fomu Shayo alisindikizwa na makada wenzake akiwamo
aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo Priscus Tarimo.
Akizungumza mbele ya umati wa
wanachama wa CCM nje ya jengo la Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Priscus
alisema ndani ya CCM hakuna kununiana.
Alisema wao kama wana CCM wanajukumu moja
la kuhakikisha kura za Rais,Wabunge na Madiwani zinamwagika.








