WAZIRI: NIKICHAGULIWA NITASHUGHULIKIA BARABARA, MIFUGO, MASOKO NA UJIRANI MWEMA ARUSHA CHINI


MOSHI-KILIMANJARO.

Diwani mteule wa Kata ya Arusha Chini, Leonard Waziri, amewashukuru wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wananchi wa kata hiyo kwa kuendelea kumuunga mkono na kumpa ushirikiano ambao umewezesha kuteuliwa tena kuwa mgombea wa nafasi ya udiwani katika uchaguzi wa mwaka huu.


Waziri alitoa kauli hiyo Agosti 25,2025 wakati wa tukio la kurejesha fomu za uteuzi kwa Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi kupitia Tume Huru ya Uchaguzi (INEC), halmashauri ya Wilaya ya Moshi Vijijini, tukio lililofanyika katika kata hiyo. 


“Kwa mujibu wa kanuni za Tume ya Uchaguzi za mwaka 2024, tunapaswa kurudisha fomu zetu si chini ya siku tatu kabla ya mwisho wa muda uliopangwa, yaani Agosti 27. Leo nimekuja kukabidhi fomu kwa ajili ya ukaguzi na kama kuna marekebisho, nipate maelekezo,” alisema Waziri. 

Diwani huyo mteule alitumia fursa hiyo kuwaeleza wananchi kuwa, endapo atachaguliwa tena kuendelea na nafasi hiyo, ana vipaumbele saba ambavyo atavisimamia kwa nguvu. 


Aliyataja kuwa ni: Ujenzi wa barabara ya Mikocheni–Chemchem, Uboreshaji wa skimu ya umwagiliaji, Ujenzi wa bwawa la kunyweshea mifugo, Kuanzishwa kwa mnada wa mifugo, Kuanzishwa kwa soko la mazao ya mbogamboga, Ujenzi wa ofisi za CCM kwenye maeneo ya matawi pamoja na Kukuza sera ya ujirani mwema ndani ya kata hiyo.

 “Wananchi wa Arusha Chini wanategemea sana kilimo na ufugaji, hivyo miradi hii inalenga kuboresha maisha yao na kuondoa migogoro ya mara kwa mara, hasa kati ya wakulima na wafugaji,” alisema Waziri. 


Katika tukio hilo, baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Mikocheni waliomsindikiza waliwasilisha kilio chao kuhusu hali mbaya ya barabara ya Mikocheni–Chemchem, wakimtaka diwani huyo kushughulikia suala hilo kwa haraka. Mkazi wa kijiji hicho, Rukia Omari, alisema: 

“Mvua zinaponyesha barabara haipitiki kabisa, hata mazao tunayolima hushindwa kusafirishwa kwa sababu ya ukosefu wa usafiri.” 


Naye Karibia Lekule aliongeza kuwa wanafunzi wamekuwa wakishindwa kuhudhuria masomo kwa sababu ya maji mengi kujaa barabarani, hali inayozuia hata kutembea kwa miguu.

 “Tunaomba viongozi walioteuliwa kugombea nafasi za ubunge na udiwani kuhakikisha wanatatua kero hii ya muda mrefu,” alisema Makore Mmari, mkazi mwingine wa kijiji hicho.








Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.