MOSHI-KILIMANJARO.
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Moshi Vijijini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Morris Makoi, ameahidi kuwa ataanza kwa kushughulikia ujenzi wa barabara ya Mikocheni–Chemchem mara tu atakapochaguliwa kuwa Mbunge wa jimbo hilo katika uchaguzi wa Oktoba 29, 2025.
Makoi ametoa kauli hiyo Agosti 25,2025, kwenye kikao cha mkutano mkuu wa CCM Kata ya Arusha Chini, ulioitishwa kwa lengo la kumtambulisha diwani mteule wa kata hiyo, Leonard Waziri.
“Barabara ni uchumi, barabara ni maendeleo. Ninatambua changamoto kubwa mnazozipitia wananchi wa Arusha Chini, hususan katika barabara ya Mikocheni–Chemchem, nikiwa mbunge kazi yangu ya kwanza ni kuhakikisha barabara hii inatengenezwa,” alisema Makoi mbele ya wajumbe wa mkutano huo.
Mbali na barabara, Makoi ametaja kuimarisha skimu ya umwagiliaji na kupunguza migogoro kati ya wakulima na wafugaji kuwa miongoni mwa vipaumbele vyake vikuu.
“Kuna changamoto kubwa katika ukanda huu, hasa migogoro baina ya wakulima na wafugaji, nitahakikisha kunajengwa miundombinu ya umwagiliaji na bwawa maalum la kunyweshea mifugo ili kutatua tatizo hilo,” amesema.
Makoi pia amewashukuru wajumbe na wananchi wa Arusha Chini kwa ushirikiano wao tangu kuanza kwa safari yake ya kisiasa hadi kuteuliwa kuwa mgombea ubunge.
“Nawashukuru sana kwa mchango wenu mkubwa. Safari hii si yangu peke yangu, ni ya wote,” amesema.Makoi.
Kwa upande wake, Diwani mteule wa Kata ya Arusha Chini, Leonard Waziri, amempongeza Makoi kwa kuteuliwa na Kamati Kuu ya CCM Taifa kuwania nafasi hiyo ya ubunge.
Waziri amemkumbusha pia juu ya ombi la shilingi bilioni 1.127 aliloliwasilisha kwenye kikao cha baraza la madiwani kilichoketi kwa ajili ya kupitisha bajeti ya mwaka 2025/2026.
Waziri amesema kwenye bajeti hiyo aliwqsilisha ombi hilo kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Mikocheni–Chemchem, akimtaka kuhakikisha fedha hizo zinatolewa ili kuondoa kilio cha muda mrefu cha wakazi wa kata hiyo.
Naye Mwenyekiti wa CCM Kata ya Arusha Chini, Furahini Bakari, ameeleza kuwa licha ya mkutano huo wa kumtambulisha diwani mteule pia ulilenga kuvunja makundi ndani ya chama na kuwaunganisha wanachama kumuunga mkono diwani aliyeteuliwa.
“Kanuni na maadili ya chama yanasema wazi kuwa mwanachama ana haki ya kugombea, lakini pia anatakiwa kukubali maamuzi ya vikao halali vya chama. Mtu yeyote anayekaidi, anakosa nidhamu na atachukuliwa hatua,” alisema Bakari.
Amesisitiza kuwa kwa sasa hakuna makundi ndani ya chama na kuwa kundi pekee linalokubalika ni CCM yenyewe, likiwa na lengo moja la kumshika mkono na kumnadi mgombea aliyepitishwa.









