JANETH LYAKURWA; AJITOSA KUGOMBEA UDIWANI KATA YA MABOGINI KUPITIA SAU, AAHIDI SHULE, MIUNDOMBINU BORA

MOSHI-KILIMANJARO.

Janeth Hugo Lyakurwa amechukua rasmi fomu ya kugombea udiwani wa Kata ya Mabogini kupitia Chama cha Sauti ya Umma (SAU), ambapo ameahidi kusimamia uboreshaji wa huduma za elimu na miundombinu ikiwa atachaguliwa kuwa diwani.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuchukua fomu hiyo, Lyakurwa alisema moja ya changamoto kubwa inayowakabili wananchi wa kata hiyo ni ukosefu wa shule ya msingi na sekondari katika Kijiji cha Shabaha, jambo linalozuia watoto kupata haki yao ya msingi ya elimu.

“Kijiji cha Shabaha hakina shule ya msingi wala sekondari. Nitahakikisha shule hizo zinajengwa ili watoto wetu wasitembee umbali mrefu kutafuta elimu,” alisema Lyakurwa.

Ameongeza kuwa pia atashughulikia miundombinu ya barabara, akieleza kuwa barabara duni zimekuwa kikwazo kikubwa kwa wakulima kusafirisha mazao yao kwenda sokoni.

“Nitashirikiana na TARURA kuhakikisha barabara zinatengenezwa, wakulima wapate urahisi wa kupeleka mazao yao sokoni na kuinua kipato chao,” alieleza.

Janeth pia amewahamasisha wananchi wa Kata ya Mabogini kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura katika uchaguzi mkuu ujao, akiwahakikishia kuwa akiwa diwani wao, atakuwa sauti ya kutatua changamoto zao kwa vitendo.

“Naomba ridhaa yenu ili niwe sauti yenu. Nikipewa nafasi nitahakikisha mambo yenu hayaishii kwenye ahadi, bali kwenye utekelezaji,” alisisitiza.

SAU imeendelea kupokea wagombea katika ngazi mbalimbali za uongozi kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu, ikisisitiza uwajibikaji na utumishi wa kweli kwa wananchi.







Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.