MOSHI-KILIMANJARO.
Isaack Kireti Kamasho amechukua rasmi fomu ya kugombea ubunge wa Jimbo la Moshi Mjini kupitia Chama cha Sauti ya Umma (SAU), huku akiahidi kuleta mageuzi ya kiuchumi, kijamii na kimazingira endapo wananchi watamchagua kuwa mwakilishi wao bungeni.
Kamasho alikabidhiwa fomu hiyo tarehe 21 Agosti 2025 na Katibu Msaidizi wa SAU Mkoa wa Kilimanjaro, Richard Shangali, katika ofisi za chama hicho zilizopo mjini Moshi.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuchukua fomu, Kamasho alisema kuwa kipaumbele chake cha kwanza ni kuinua uchumi wa wananchi wa Moshi Mjini, hasa wa kipato cha chini, pamoja na kuimarisha demokrasia ya kweli ambayo inawapa wananchi nafasi ya kushiriki kikamilifu katika maamuzi ya maendeleo ya eneo lao.
“Nataka Moshi Mjini iwe kitovu cha maendeleo jumuishi. Uchumi wa watu wetu lazima uimarike, na hilo linawezekana kupitia sera shirikishi na demokrasia ya kweli,” alisema Kamasho.
Kamasho pia alisisitiza dhamira yake ya kulinda mazingira kwa njia ya kupanda miti ya matunda, akisema hatua hiyo itasaidia si tu kupambana na mabadiliko ya tabianchi bali pia kukabiliana na utapiamlo miongoni mwa watoto na familia masikini.
Aidha, aliweka bayana kuwa atasimama pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika jitihada za kuhakikisha wananchi wa kipato cha chini wanapata nishati safi ya kupikia, kama njia ya kulinda afya zao na mazingira.
“Nitahakikisha gesi ya kupikia inakuwa nafuu zaidi kwa kila Mtanzania. Mtungi mdogo wa gesi uweze kujazwa kwa Shilingi 5,000 tu – hili linawezekana tukiamua kwa vitendo,” alisisitiza.
Kamasho ameungana na wagombea wengine wa SAU katika mchakato wa kugombea nafasi za uongozi, huku chama hicho kikitoa wito kwa wagombea wake kuzingatia masuala ya msingi ya wananchi badala ya siasa za makundi au maslahi binafsi.






