MZEE WA MIAKA 70 AJITOSA KUGOMBEA UBUNGE JIMBO LA SIHA KUPITIA SAU, AAHIDI KUTETEA WAKULIMA, WAZEE

MOSHI-KILIMANJARO.

Mzee Mdoe Yambazi Azaria, mwenye umri wa zaidi ya miaka (70), amejiunga rasmi na kinyang'anyiro cha ubunge wa Jimbo la Siha kupitia Chama cha Sauti ya Umma (SAU), baada ya kuchukua fomu ya kugombea Agosti 22, 2025, katika ofisi za chama hicho zilizopo mkoa wa Kilimanjaro.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuchukua fomu hiyo, Mzee Azaria alisema kuwa ameamua kuwania nafasi hiyo ili kuwa sauti ya wanyonge, hususan wakulima wasio na ardhi na wazee wanaokosa huduma za afya.

“Kama wananchi wa Siha watanipa ridhaa ya kuwa mbunge wao, nitahakikisha wale wasio na ardhi wanapata maeneo ya kulima, kwa sababu ardhi ni haki yao ya msingi,” alisema.

Mzee Azaria aliongeza kuwa wazee wengi hawana uwezo wa kugharamia matibabu, na kwamba moja ya ajenda yake kuu ni kuhakikisha wazee wanapata bima ya afya itakayowawezesha kupata matibabu bila kulipia.

“Wazee wetu wameitumikia nchi hii kwa miaka mingi, sasa ni wakati wao kuheshimiwa kwa vitendo kupitia huduma bora za afya, nitahakikisha hili linafanikiwa,” alisisitiza.

Katika kuonesha uzalendo wake kwa jimbo hilo, Mzee Azaria alitoa kauli iliyowasisimua wengi:

"Mtu yeyote anayestahili kuwa mbunge wa Jimbo la Siha lazima aiote Siha. Huwezi kuiota Siha kama hulali Siha.”

Mzee huyo ambaye ni mkongwe kisiasa na kijamii, alisema amekuwa akiishi na kushuhudia changamoto za wananchi wa Siha kwa muda mrefu, hivyo anaelewa kwa undani mahitaji yao halisi.

Katibu Msaidizi wa Chama cha SAU Mkoa wa Kilimanjaro, Richard Shangali, alimkabidhi rasmi fomu ya kugombea na kumpongeza kwa uamuzi wake wa kujitokeza katika uchaguzi huo kama kiongozi mwenye uzoefu na dhamira ya kweli ya kuwatumikia wananchi.

Chama cha Sauti ya Umma (SAU) kimeendelea na mchakato wa kupokea wagombea mbalimbali kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu, kikiwataka wagombea wake kuzingatia maslahi ya wananchi na si maslahi binafsi.





Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.