MOSHI-KILIMANJARO.
Mgombea Udiwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Kata ya Kilimanjaro, Mohamed Salim Gulamhusein, ameishukuru CCM kwa kumuamini na kumrejesha katika nafasi ya uteuzi wa kugombea udiwani katika uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani.
Gulamhusein alitoa kauli hiyo Agosti 22, 2025, alipokuwa akizungumza na wanachama wa chama hicho waliofika kumpa pongezi mara baada ya kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo.
Amesema uteuzi huo ni heshima kubwa kwake, na kwamba ni matokeo ya imani ya chama pamoja na wanachama wa Kata ya Kilimanjaro waliomuunga mkono.
“Nawashukuru sana wananchi wa Kata ya Kilimanjaro kwa kuniunga mkono, leo nimechukua rasmi fomu ya kugombea udiwani, ambazo nimekabidhiwa na Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi (INEC), Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Richard Rumisha,” alisema Gulamhusein.
Ameongeza kuwa anafahamu changamoto zinazowakabili wananchi wa kata hiyo kwa sababu yeye ni mkazi wa eneo hilo, hivyo amejiandaa kutekeleza vipaumbele alivyowaahidi.
"Nawafahamu wanachama wa CCM na wananchi wa kata hii, mimi ni mzaliwa na mkazi wa hapa. Changamoto zenu ni zangu. Nimeahidi na nitatekeleza vipaumbele kwa maslahi ya wote,” alisisitiza.
Gulamhusein pia alieleza kuguswa na mapokezi aliyoyapata kutoka kwa wanachama na wananchi waliojitokeza kwa wingi kumsindikiza kuchukua fomu, akisema upendo huo unaonesha imani waliyonayo kwake kama kiongozi wa baadaye.
Aidha, alitumia fursa hiyo kumpongeza Mwenyekiti wa CCM Taifa, Mhe. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Kamati Kuu ya Chama kwa uamuzi wa kuridhia jina lake kurejeshwa kwenye mchakato wa uteuzi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Kata ya Kilimanjaro, Barnaba, aliwapongeza wanachama na wananchi kwa kujitokeza kwa wingi kumsindikiza mgombea huyo, akisema hatua hiyo inaonesha mshikamano na umoja ndani ya chama.
















