PAUL GEORGE MAILE WA CCM ACHUKUA FOMU INEC KATA YA SOWETO

MOSHI – KILIMANJARO.

Zikiwa ni siku chache tangu kufunguliwa rasmi kwa mchakato wa uchukuaji fomu za kugombea nafasi za udiwani kupitia Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Agosti 18,2025 Paul George Maile, diwani mteule wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Soweto, alihitimisha jukumu lake la kikatiba kwa kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo.

Msafara wa Maile ulianzia katika ofisi za CCM Kata ya Soweto, ukisindikizwa kwa shangwe na nderemo kutoka kwa viongozi wa chama, wananchi, vikundi vya ngoma za asili, pikipiki (bodaboda), na bajaji, hadi katika ofisi za Serikali ya Kata ya Soweto, ambako ndiko fomu hizo hutolewa na INEC.

Mara baada ya kufika katika ofisi hizo, Maile alipokelewa rasmi na Niwael Elirehema Mnkeni, ambaye ni Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi katika Kata hiyo, na kukabidhiwa fomu kama ishara ya kutimiza moja ya hatua muhimu katika mchakato wa kugombea nafasi ya udiwani.

Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu, Maile alieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya utii kwa Katiba na utaratibu uliowekwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kwa wagombea wote waliopewa ridhaa ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kupitia vyama vyao.

"Nakishukuru chama changu CCM kwa imani kubwa mliyonipa kwa kuniteua kuwa mgombea wa udiwani wa Kata ya Soweto, hili ni deni kubwa kwangu na nitahakikisha ninalilipa kwa kufanya kazi kwa uadilifu, weledi, na kujitoa kwa ajili ya wananchi,” alisema Maile.

Aidha Maile aliwataka wananchi wa Kata ya Soweto kujitokeza kwa wingi kwenye mikutano ya kampeni itakapoanza rasmi, ili kusikiliza sera na mipango ya wagombea kwa ajili ya maendeleo ya kata hiyo.

Hatua ya Maile ya kuchukua fomu inajumuishwa katika mfululizo wa wagombea wa CCM wanaoendelea na mchakato wa kikatiba wa kuwania nafasi ya udiwani ndani ya Wilaya ya Moshi Mjini kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.










Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.