MOSHI – KILIMANJARO.
Mgombea udiwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Mawenzi, Apaikunda Naburi, amechukua fomu ya kugombea nafasi hiyo kupitia Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) katika ofisi za Serikali ya Kata ya Mawenzi, tayari kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Naburi ni miongoni mwa wanasiasa wenye rekodi ya muda mrefu wa utumishi katika Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, akiwa na historia ya kuhudumu katika nafasi hiyo kwa vipindi mbalimbali tangu mwaka 2000.
Mwaka 2000, Naburi alianza kuwa diwani wa viti maalum kupitia CCM na alihudumu hadi mwaka 2010. Katika uchaguzi wa mwaka 2015, alijitosa tena kuwania nafasi ya diwani wa Kata ya Mawenzi lakini hakufanikiwa, baada ya kushindwa na Hawa Mushi wa CHADEMA.
Hata hivyo, mwaka 2018, kufuatia kifo cha aliyekuwa diwani wa kata hiyo, uchaguzi wa marudio ulifanyika ambapo Naburi aliibuka mshindi na kuchukua tena nafasi hiyo ya udiwani, nafasi aliyohudumu hadi mwaka huu wa uchaguzi, 2025.
Kwa mwaka huu wa uchaguzi, Apaikunda Naburi amerudi tena kutetea nafasi yake hiyo, ambapo katika kura za maoni ndani ya CCM aliongoza, jambo lililomuwezesha kupitishwa na Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kilimanjaro kuendelea na hatua za mbele katika mchakato wa uchaguzi.
Kati ya wagombea 163 waliowasilisha nia ya kugombea nafasi ya udiwani kupitia CCM katika Wilaya ya Moshi Mjini, ni wagombea 21 pekee waliopitishwa na Halmashauri Kuu ya Mkoa, akiwemo Apaikunda Naburi, ambaye sasa anaendelea na kampeni kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.















