WILLY TULLY ACHUKUA FOMU INEC KIBORILONI

MOSHI – KILIMANJARO

Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Moshi Mjini, mkoani Kilimanjaro, kimefungua rasmi pazia la uchukuaji fomu za kugombea nafasi ya udiwani kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, kuanzia Agosti 17, 2025.

Mnamo Agosti 18, 2025, mgombea wa CCM kwa nafasi ya udiwani Kata ya Kiboriloni, Willy Tully, alifika katika ofisi za Serikali za Kata hiyo kuchukua fomu kutoka kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), ikiwa ni sehemu ya mchakato wa kuelekea uchaguzi huo.

Tukio hilo liliongozwa na viongozi wa CCM wa ngazi ya kata, likisindikizwa na shamrashamra kutoka kwa wanachama wa chama hicho, wapenzi wa CCM, pamoja na baadhi ya wananchi wa Kiboriloni waliojitokeza kuonesha mshikamano na uungwaji mkono kwa mgombea huyo.

Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu, Willy Tully alisema ameamua kuwania nafasi hiyo ili kushirikiana na wananchi wa kata hiyo kuendeleza na kusimamia utekelezaji wa sera na ilani ya Chama cha Mapinduzi, chini ya Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dk. Samia Suluhu Hassan, ambaye pia ni mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

"Nakishukuru chama changu CCM kwa kuniamini na kuniteua kuwa mgombea wa udiwani wa Kata ya Kiboriloni. Leo hii, Agosti 18, 2025, nimefika katika ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) zilizoko hapa Kiboriloni na kukabidhiwa fomu na Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi, ndugu Rashid A. Rashid,” alisema Tully.

Aidha, aliongeza kuwa baada ya kuchukua fomu hiyo ataendelea na taratibu nyingine zinazotakiwa kikanuni, huku akiwaomba wananchi wa Kiboriloni na Watanzania wote kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, 2025, ili kutekeleza haki yao ya kikatiba kwa kupiga kura.

Katika muktadha wa kisiasa, Jimbo la Moshi Mjini limekuwa na historia ya kuongozwa na vyama vya upinzani tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1995.

Katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka huo, Antony Komu alishinda ubunge kupitia NCCR-Mageuzi kabla ya kujiunga na CHADEMA. Kuanzia mwaka 2000 hadi 2015, jimbo hilo liliongozwa na marehemu Philemon Ndesamburo kupitia CHADEMA, na baadaye mwaka 2015 nafasi hiyo ilichukuliwa na Japhary Michael kupitia chama hicho hicho hadi mwaka 2020.

Hata hivyo, katika Uchaguzi Mkuu wa 2020, CCM kupitia mgombea wake Priscus Jacob Tarimo, ilifanikiwa kulichukua jimbo hilo kwa mara ya kwanza katika kipindi hicho cha vyama vingi, na kulifanya kuwa chini ya CCM kwa kipindi cha 2020 hadi 2025.

Kwa mujibu wa duru mbalimbali za kisiasa, Kata ya Kiboriloni ilikuwa miongoni mwa maeneo ya mwisho kubaki chini ya upinzani kwa muda wa miaka 25. Hata hivyo, mwelekeo wa uchaguzi wa mwaka 2025 unaonesha kwamba kata hiyo huenda ikarejea rasmi mikononi mwa CCM, hatua inayochukuliwa kama ishara ya mabadiliko ya kisiasa katika Wilaya ya Moshi Mjini.









Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.