MGOMBEA UDIWANI KATA YA KORONGONI ISSA JUMA ACHUKUA FOMU, ATOA SHUKRANI KWA TUME YA UCHAGUZI

MOSHI-KILIMANJARO.

Mgombea udiwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Korongoni, Issa Elias Juma, Agosti 18,2025, amechukua rasmi fomu ya kugombea nafasi hiyo kutoka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kupitia ofisi za Serikali ya Mtaa zilizopo Kata ya Korongoni.

Juma alifika katika ofisi hizo majira ya saa nne asubuhi, akisindikizwa na msafara wa vijana wa hamasa, waendesha bodaboda, pamoja na matarumbeta, hali iliyoashiria hamasa kubwa kwa wananchi wa Kiusa kuelekea uchaguzi huo.

“Tayari nimefika kwenye ofisi ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi zilizopo hapa katika ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Korongoni, na kukabidhiwa fomu na msimamizi msaidizi wa Uchaguzi, nitaenda kuzijaza na kuzirudisha mapema,” alisema Juma baada ya kukabidhiwa fomu.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Wilaya ya Moshi Mjini, Athuman Ally Mfuchu, alithibitisha kuwa jumla ya madiwani 21 wamechaguliwa kupeperusha bendera ya CCM katika kata mbalimbali za wilaya hiyo kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025. 

“Madiwani hawa ni wale walioongoza kwenye kata zao kupitia mchakato wa kura za maoni, pamoja na baadhi ya madiwani wa viti maalum walioteuliwa kwa mujibu wa taratibu za chama, wapo tayari kuingia katika kinyang’anyiro na wagombea wa vyama vingine,” alisema Mfuchu.

Mchakato wa utoaji wa fomu unaendelea kwa wagombea wa CCM kote nchini, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mwisho kuelekea kampeni rasmi za uchaguzi mkuu mwaka huu.








Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.