KHALID SHEKOLOA, ACHUKUA FOMU YA UDIWANI KATA YA KIUSA, ATOA SHUKRANI KWA WANANCHI

MOSHI-KILIMANJARO.

Mgombea udiwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Kiusa, Khalid Shekoloa, Agosti 18, 2025 amechukua rasmi fomu ya kugombea nafasi hiyo kutoka kwa msimamizi msaidizi wa Uchaguzi wa Kata ya Kiusa, huku akiwashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi kumsindikiza.

Shekoloa, ambaye aliwasili katika ofisi za Serikali za kata hiyo akiwa ameandamana na wana-CCM na wafuasi wake, alieleza kufurahishwa na mshikamano uliooneshwa na wananchi wa kata hiyo, katika kumuunga mkono katika hatua hiyo muhimu ya mchakato wa uchaguzi mkuu.

“Nawashukuru sana wananchi wa kata ya Kiusa, kwa kujitokeza kwa wingi kuniunga mkono na kunisindikiza kuchukua fomu, huu ni ushahidi wa imani kubwa waliyonayo kwa CCM na kwa utekelezaji wa Ilani ya chama chetu,” alisema Shekoloa mara baada ya kukabidhiwa fomu.

Akizungumza na wana-CCM waliomsindikiza, Khalid Shekoloa, alisema anaamini utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025 umeleta maendeleo makubwa yanayoonekana katika jamii, na kuwa kazi kubwa sasa ni kwenda kuiuza Ilani hiyo mpya kwa wananchi ili kuhakikisha CCM inaendelea kushika dola.

“Jukumu lililopo mbele yetu ni kuhakikisha tunakwenda kutafuta kura za kishindo kwa Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Mbunge atakayeteuliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi,” aliongeza Shekoloa.









Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.