MOSHI-KILIMANJARO.
Mgombea udiwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Mfumuni, Stuart Nathael, Agosti 17,2025, amechukua rasmi fomu ya kugombea nafasi hiyo katika ofisi za Serikali za kata hiyo, hatua inayofuatia baada ya kupitishwa na chama chake kupitia mchakato wa kura za maoni.
Fomu hizo zimekabidhiwa na Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi wa Kata ya Mfumuni, Isihaka Juma, mara baada ya Nathael kuwasili katika ofisi hizo majira ya alasiri akiwa ameandamana na msafara mkubwa wa wafuasi wa CCM, wananchi, pikipiki na bajaji, hali iliyopamba shamrashamra za tukio hilo.
"Nimefika kwenye ofisi za serikali na kupokelewa na msimamizi msaidizi wa uchaguzi ambaye amenikabidhi fomu, nakwenda kuzijaza kwa umakini na kuzirudisha mapema ili kazi iendelee," alisema Nathael.
Agosti 16, 2025, CCM Wilaya ya Moshi Mjini iliwakabidhi madiwani wake wateule barua rasmi za uteuzi, ikiwa ni hatua ya mwisho baada ya mchakato wa ndani wa chama kupata wagombea waliopitishwa na Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kilimanjaro, kupeperusha bendera ya CCM katika kata mbalimbali.
Mchakato huu unaendelea kuonesha mshikamano na umoja mkubwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
![]() |

.jpg)





