MOSHI-KILIMANJARO.
Diwani mteule wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Ng’ambo, Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro, Gadiel Mrema, Agosti 17,2025, amechukua fomu ya kugombea nafasi ya udiwani kupitia Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) katika ofisi za Serikali zilizopo katika kata hiyo.
Hatua hiyo imefuatia kukamilika kwa mchakato wa kura za maoni ndani ya chama hicho, ambapo, Mrema aliibuka mshindi na kuwa mgombea rasmi wa CCM kwa nafasi ya udiwani katika kata ya Ng’ambo.
Mrema aliwasili katika ofisi za kata akisindikizwa na umati wa wana-CCM na wakazi wa Ng’ambo waliomsindikiza kwa shangwe, nderemo na vifijo kutoka nyumbani kwake hadi kwenye ofisi hizo.
Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu, Mrema alisema “Nimefarijika kuchukua fomu za kugombea nafasi ya udiwani kwa kata yangu ya Ng’ambo, ninawashukuru sana wananchi wangu kwa kujitokeza kwa wingi kunisindikiza, nitazijaza kwa umakini na kuzirejesha mapema kama taratibu zinavyoelekeza.”
Tukio hilo limeendelea kudhihirisha mshikamano na hamasa ndani ya CCM katika kuelekea Uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29,mwaka huu.







