TUKACHARU RAU FOREST CHARITY MSIMU WA TATU YAZINDULIWA


MOSHI-KILIMANJARO.

Tukio la TUKACHARU RAU FOREST CHARITY msimu wa tatu limezinduliwa rasmi Agosti 15,2025 katika hafla iliyofanyika kwenye eneo la Mbega Campsite, ndani ya Msitu wa Asili wa Rau, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro. 

Tukio hilo limeendelea kujizolea umaarufu mkubwa kutokana na mchango wake katika kuhamasisha utalii wa ndani sambamba na kuhifadhi mazingira na kusaidia jamii yenye uhitaji.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, aliupongeza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa jitihada zao za kuendeleza hifadhi hiyo na kuifanya kuwa kivutio muhimu cha utalii katika mkoa wa Kilimanjaro.

Alisisitiza kuwa serikali inaendelea kuunga mkono jitihada za kuimarisha utalii wa ndani, ambao una nafasi kubwa ya kuchangia uchumi wa taifa na kuboresha maisha ya wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya hifadhi.


“Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa mdau namba moja katika uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya sekta ya utalii nchini, juhudi zake hizo zimechangia ongezeko kubwa la watalii na mapato katika sekta hii muhimu,” alisema Mnzava.

Aidha, mkuu huyo wa wilaya alimpongeza Mhifadhi wa TFS Wilaya ya Moshi, Godfrey Ullomi, na timu yake kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutunza msitu huo wa asili.

Kwa upande wake, Mhifadhi Ullomi alisema tangu kuanzishwa kwa Tukacharu Rau Forest Charity mwaka 2023, kumekuwa na ongezeko kubwa la watalii wanaotembelea msitu huo.

“Msimu wa kwanza tulipokea watalii 6,500, msimu wa pili tukafikia 11,800, na kwa msimu huu wa tatu tunatarajia kuvunja rekodi kwa kufikia watalii 20,000,” alisema Ullomi kwa matumaini makubwa.

Aliongeza kuwa idadi ya washiriki wa tukio hilo imeendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka, jambo linaloonyesha mwitikio mkubwa kutoka kwa jamii.

 “Msimu wa kwanza tulikuwa na washiriki 360, msimu wa pili wakafikia 670, tunaamini msimu huu tutavuka idadi hiyo,” alifafanua.

Naye Mratibu wa tukio hilo, Rosemary Didas, alisema lengo kuu la Tukacharu ni kuhamasisha utalii wa ndani huku pia likiwa ni jukwaa la kuchangisha rasilimali kwa ajili ya kusaidia makundi maalum katika jamii.

“Mapato yanayopatikana kutoka kwenye tukio hili yatatumika kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu, watoto yatima, watu wenye ulemavu na wazee wasiojiweza,” alisema Didas.

Tukio la Tukacharu limekuwa mfano wa kuigwa kwa kuunganisha uhifadhi wa mazingira, utalii endelevu, na huduma kwa jamii, likiwa na mchango chanya kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika Mkoa wa Kilimanjaro.












Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.