TUKACHARU SEASON 3; KUNUFAISHA WATU WENYE MAHITAJI MAALUM


MOSHI-KILIMANJARO.

Watu wapatao 170 kutoka katika makundi yenye uhitaji maalum wanatarajiwa kunufaika na misaada mbalimbali kupitia tukio maalum la utalii wa kijamii litakalofanyika kesho, Agosti 15, ndani ya Msitu wa Hifadhi ya Asili ya Rau, uliopo Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Tukio hilo linafanyika chini ya mwamvuli wa Rau Forest Tukacharu Charity Tour, ambalo kwa mwaka huu linaingia msimu wake wa tatu tangu kuanzishwa kwake.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Agosti 14,2025, Mratibu wa tukio hilo, Rosemary Didas, alisema lengo kuu la msimu huu ni kutumia mapato ya utalii kutoka msitu huo kusaidia watu wenye  mahitaji maalumu kama sehemu ya kurudisha kwa jamii.

“Mwaka huu tumejipanga kuwafikia watu 170 kutoka makundi mbalimbali kama wazee, watu wenye ulemavu, watoto yatima na wengine wenye mahitaji maalum, kwa kuwapatia misaada kama chakula, vifaa vya matibabu na kulipia gharama za matibabu,” alisema Rosemary.

Aidha, alibainisha kuwa mbali na misaada hiyo, watu hao pia watapata fursa ya kutembelea Msitu wa Rau kama sehemu ya kujumuika kijamii na kupata burudani, vivyo hivyo kama wageni wa kawaida kutoka ndani na nje ya nchi.

"Lengo letu ni kuhakikisha kuwa hata wale wenye changamoto mbalimbali za kijamii wanapata nafasi ya kufurahia vivutio vya utalii vilivyopo nchini mwao,” aliongeza.

Rosemary pia aliwataka Watanzania kujenga utamaduni wa kutembelea vivutio vya ndani ikiwemo Msitu wa Rau, ambao alisema ni kivutio adimu kwa kuwa ni moja ya misitu ya asili inayopatikana katikati ya mji katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Kwa upande wake, Mratibu Msaidizi wa tukio hilo, Cleophas Simchimba, alisema tukio la mwaka huu litakuwa la kipekee likihusisha shughuli mbalimbali zikiwemo matembezi ya pekupeku ndani ya msitu huo.

“Matembezi ya pekupeku yataletwa kama njia ya kipekee ya kuhamasisha utalii wa ndani na kuyaelewa mazingira ya msitu kwa ukaribu zaidi, matembez haya yataongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Moshi Godfrey Mnzava, ” alisema Simchimba.

Aliongeza kuwa shughuli nyingine zitahusisha mbio za kilomita tano na kumi pamoja na mashindano ya kuendesha baiskeli, ambayo yamepewa jina la “Mbio Bila Kutoka Jasho” kutokana na hali ya ubaridi inayopatikana ndani ya Msitu wa Rau.

Tukio hili limebeba ujumbe wa kijamii na kimazingira, likiwa pia ni sehemu ya kutangaza utalii wa ndani na kuonesha umuhimu wa kuenzi mazingira ya asili kama urithi wa Taifa.








Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.